Hospitali elfu moja za Marekani zimejaa wagonjwa, haziwezi tena kutoa huduma
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64802-hospitali_elfu_moja_za_marekani_zimejaa_wagonjwa_haziwezi_tena_kutoa_huduma
Mkurugenzi wa Kitivo cha Usalama wa Afya cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins ametangaza kuwa, sasa hivi hospitali elfu moja zimeshajaa wagonjwa wa COVID-19 nchini humo na hazina tena uwezo wa kupokea wagonjwa zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2020 22:53 UTC
  • Hospitali elfu moja za Marekani zimejaa wagonjwa, haziwezi tena kutoa huduma

Mkurugenzi wa Kitivo cha Usalama wa Afya cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins ametangaza kuwa, sasa hivi hospitali elfu moja zimeshajaa wagonjwa wa COVID-19 nchini humo na hazina tena uwezo wa kupokea wagonjwa zaidi.

Thomas Inglesby amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Fox News ambayo iko karibu sana na chama cha Republican cha rais wa Marekani, Donald Trump na kuongeza kuwa, karibu hospitali elfu moja zilijaa wiki hii na sasa hivi zina upungufu mkubwa wa vifaa vya matibabu au wakati wowote zitakumbwa na mgogoro huo hasa kwa kuzingatia kuwa wimbi la wagonjwa wa COVID-19 linazidi kumiminika kwenye hospitali za nchi hiyo.

Inglesby aidha amesema, wimbi jipya la kupanda na kuongezeka wagonjwa wa corona ndio kwanza limeanza nchini Marekani.

Donald Trump anashutumiwa vikwali kwa kuwasababishia Wamarekani maafa makubwa ya corona

 

Mkurugenzi huyo wa Kitivo cha Usalama wa Kiafya cha Chuo Kikuu cha Hopkins cha Marekani ameongeza kuwa, siasa zilizochukuliwa na serikali ya Donald Trump katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni ndizo zilizopelekea kuweko idadi kubwa kiasi chote hicho ya wagonjwa wa corona na kadiri siku zinavyopita ndivyo wimbi la wagonjwa wa corona linavyozidi kuwa kubwa.

Rais wa Marekani, Donald Trump anashutumiwa vikali kwa kuwasababishia maafa makubwa wananchi wa Marekani kutokana na kuufanyia istihzai za kila namna ugonjwa huo hatari. Itakumbukwa kuwa, mara kwa mara Trump ameonekana akiwafanyia istihzai wagonjwa wa corona kama vile kuwataka wanywe au wadungwe mada za sumu za kuua kirusi cha corona. Aidha mara kwa mara Trump ameonekana akijifanya daktari bingwa na kuwaainishia madaktari dawa "mujarrab" za corona bila ya kuwa na ushahidi wowote wa kitaalamu.