May 06, 2016 08:01 UTC
  • Waziri Mkuu wa Uturuki athibitisha kuacha uongozi wa chama tawala

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoğlu, ametangaza rasmi kuwa ataacha uongozi wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi (AKP) na hivyo kulazimika pia kuachia madaraka ya Uwaziri Mkuu.

Davutoğlu amelazimika hatimaye kuchukua uamuzi huo ikiwa ni kusalimu amri mbele ya takwa la Rais Recep Tayyip Erdoğan la kutaka kuongezwa mamlaka ya rais .

Akizungumza mbele ya wanachama wa chama tawala hapo jana, Waziri Mkuu wa Uturuki ametetea uongozi na utendaji wake akisema ameweza kukilinda chama cha AKP katika kipindi cha dhoruba za kisiasa.

Sambamba na kusisitiza utiifu wake kwa Rais Erdoğan, Waziri Mkuu wa Uturuki amesema serikali "imara" ya chama cha Uadilifu na Ustawi itaendelea na harakati yake.

Aidha ameongeza kuwa kuanzia sasa katu hatotoa kauli yoyote ya kumkosoa Erdoğan.

Ahmet Davutoğlu anajiengua katika uongozi wa chama tawala nchini Uturuki katika hali ambayo nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kali katika uga wa siasa, mgogoro wa wakimbizi na harakati za kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria.../

Tags