Obama: Siasa zangu ndizo zitakazoendelezwa na Joe Biden
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65119-obama_siasa_zangu_ndizo_zitakazoendelezwa_na_joe_biden
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amekiri kwamba siasa za serikali ya Joe Biden, rais mteule wa nchi hiyo zitakuwa zile zile alizokuwa nazo yeye wakati wa uongozi wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2020 23:22 UTC
  • Obama: Siasa zangu ndizo zitakazoendelezwa na Joe Biden

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amekiri kwamba siasa za serikali ya Joe Biden, rais mteule wa nchi hiyo zitakuwa zile zile alizokuwa nazo yeye wakati wa uongozi wake.

Gazeti la Independent limemnukuu Obama akisema hayo na kuongeza kuwa, Donald Trump ameangamiza juhudi zake zote lakini Joe Biden na naibu wake Kamala Harris, wanaweza kuendeleza siasa zake.

Rais huyo wa zamani wa Marekani ameongeza kuwa, mpango wake wa afya maarufu kwa jina la "Obama Care" umekumbwa na vizuizi na vikwazo vingi katika kipindi chote cha utawala wa Donald Trump, lakini bado unaweza kuendelezwa na serikali ijayo ya nchi hiyo.

Kabla ya hapo pia, Barack Obama alimlaumu vikali Donald Trump kwa siasa zake za mambo ya nje na kusema kuwa, dunia ingali inajiuliza, vipi itaiamini Marekani katika masuala kama ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na makubaliano ya Paris?

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Rais huyo wa zamani wa Marekani vile vile amesema, Joe Biden ana nia ya kurejea haraka kwenye makubaliano ya hali ya hewa ya Paris na mapatano ya kimataifa na nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, imani ya walimwengu iliyovurugwa kikamilifu na Donald Trump, haiwezi kurejea kwa usiku mmoja.

Wakati wa urais wa Donald Trump, wafuasi wa chama cha Republican wamefanya juhudi kubwa za kuufuta kabisa mpango wa afya wa Barack Obama yaani "Obama Care" hata hivyo walikwamishwa na Baraza la Congress la nchi hiyo.

Pamoja na hayo Trump alifanikiwa kuifuta kikamilifu sheria ya kuwasaidia watoto wa raia wa kigeni maarufu kwa jina la "Dream Act."