Familia za wanajeshi wa Marekani zinahitajia misaada ya chakula
Maafisa wa kijeshi wa Marekani wanaeleza kuwa, familia za wanajeshi nchini humo zinahitajia misaada ya chakula kutokana na kuenea maambukizi ya virusi vya corona.
Maafisa wa jeshi la Marekani wametangaza kuwa, kuenea maambukizi ya virusi vya corona nchini humo kumepelekea familia nyingi za wanajeshi katika wiki za karibuni kuelekea katika kambi za kijeshi kwa ajili ya kupata chakula.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa katika tovuti ya gazeti la New York Times, kambi ya Fort Bragg ambayo ni kambi kubwa zaidi ya kijeshi nchini Marekani mwaka huu imekabiliwa na ongezeko la asilimia 40 ya maombi ya kupatia misaada ya chakula kutoka kambi hiyo. Aidha imeelezwa kuwa maombi yanayotumwa katika mtandao kwa jina la (AmericaServes) na familia za wanajeshi wa Marekani kwa ajili ya kupatiwa misaada ya chakula yamekuwa mengi sana kuwahi kushuhudiwa katika historia ya utendaji kazi wa mtandao huo.
Hali hiyo ya mambo imezisibu familia za wanajeshi wenye kipato cha chini na wale ambao wenzao wamepoteza ajira; na wakati huo huo uwezekano wa watu hao kupata kazi mpya umetajwa kuwa mdogo sana. Weledi wa mambo wanasema kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imefanya kila linalowezekana kuficha hali hiyo ya mambo inayozikabili familia za wanajeshi wa nchi hiyo. Wakati huo huo taasisi za kusaidia watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula zinasema kuwa, wanajeshi wastaafu wa Marekani pia wana hali kama hiyo; na wamekuwa wakihitaji kupewa misaada ya chakula tangu kuenea janga la corona nchini humo.