Jan 11, 2021 13:11 UTC
  • Kuanza mwenendo wa kusailiwa Trump

Hujuma ya tarehe 6 mwezi huu ya wakereketwa na wafuasi sugu wa Rais Donald Trump katika Congress ya Marekani imezua radiamali kali katika nchi hiyo na sasa Wamarekani wanataka rais huyo achukuliwe hatua za kisheria, na tayari Wademokrat wameanzisha mwenendo wa kusailiwa kwake bungeni.

Nancy Pelosi, Spika wa Congress ya Marekani amewaandikia barua wajumbe wa bunge hilo akiwaambia kwamba wiki hii wanapaswa kuwasilisha muswada ambao utamtaka Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani na mawaziri wa serikali wamfute kazi Trump katika kipindi cha masaa 24, na hilo litatimia kwa mujibu wa marekebisho ya 25 yaliyofanyiwa katiba ya nchi hiyo.

Katika sehemu nyingine ya barua hiyo, Pelosi amesema kwamba muswada huo utapigiwa kura ima leo au kesho Jumanne na kwamba kama Pence atakataa kuutekeleza basi bunge la Congress halitakuwa na budi ila kumsaili Trump siku ya Jumatano.

Wademocrat wanategemea marekebisho hayo ya katiba ambayo yanampa makamu wa rais na baraza la mawaziri uwezo wa kumuuzulu rais iwapo watahisi kwamba hana tena uwezo wa kutekeleza rasmi majukumu yake ya kuongoza nchi. Pamoja na hayo lakini inaonekana kuwa itakuwa vigumu kwa Pence na mawaziri wa serikali kumfuta kazi Trump kwa kutilia maanani kwamba ni siku 9 tu zimebaki kabla ya kumalizika rasmi utawala wa Trump huko White House. Kwa mtazamo wa Warepublican, hatua hiyo itazidisha tu mvutano katika jamii ya Marekani na kuongeza tofauti za kisiasa kati ya wapinzani na waungaji mkono wa kiongozi huyo mwenye utata, licha ya kuongezeka nchini miito ya kutaka auzuliwe.

Nancy Pelosi (kushoto)

Robert Reich, waziri wa zamani wa leba wa Marekani ameandika kwamba wakati rais wa nchi anapowachochea waasi wenye silaha kuvuka mipaka ya Congress na kutishia usalama wa waliomo ili aendelee kubakia madarakani, hatua kama hiyo huwa si jingine bali ni jaribio la mapinduzi, hivyo anapaswa kuuzuliwa, kukamatwa na kuhukumiwa.

Kwa msingi huo ni wazi kuwa Wademokrat watamsaili Trump bungeni. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba kwa mujibu wa katiba ya Marekani, mwenendo wa kusailiwa rais wa Marekani huanza kwa kutolewa tuhuma dhidi yake. Kwa mujibu wa katiba hiyo rais wa nchi anaweza kuuzuliwa kutokana na tuhuma kama hiana, ulaji rushwa au jinai kubwa na vile vile kutoka nje ya mkondo wa sheria. Inaonekana kuwa Wademokrat pia wanataka kumuuzulu Trump kutokana na tuhuma kama vile za kuchochea, ghasia, uasi na kuvunja sheria. kwa msingi huo ni wazi kuwa Trump atakuwa rais wa kwanza kuwahi kusailiwa mara mbili katika historia ya Marekani. Kabla ya hapo tayari alikuwa amesailiwa na Congress kuhusiana na kadhia ya Ukrainegate lakini akaponea chupuchupu kutokana na upinzani wa Seneti ambayo inadhibitiwa na chama chake cha Republican.

Congress ya Marekani

Sasa Wademokrat wamepanga kumsaili tena kutokana na hatua yake ya kuchochea waasi na wafuasi wake sugu waivamie Congress, jambo lililopelekea watu watano kupoteza maisha. Kinyume na ilivyo katika bunge la Seneti, muswada wa kumsaili Trump unatazamiwa kupasisjwa kwa haraka katika Congress kwa kutilia maanani kwamba bunge hilo linadhibitiwa na Wademokrat. Inaonekana kuwa kwa kuzingatia kuwa hakuna wakati maalumu uliowekwa kwa ajili ya kutekelezwa suala hilo, Pelosi anakusudia  kuwasilisha muswada huo katika Seneti, baada ya kupita siku 100 za urais wa Joe Biden. Kwa kuzingatia kuwa wagombea wa chama cha Democrat wameshinda katika uchaguzi wa jimbo la Georgia, bunge la Seneti katika kipindi hicho litakuwa na wingi wa kura kwa manufaa ya Wademokrat na hivyo kutoa uwezekano wa kusailiwa na kuhukumiwa Trump, na hasa ikitiliwa maanani kwamba baadhi ya Warepublican wamekerwa na hatua ya Trump kuchochea kwa makusudi hujuma ya wahuni dhidi ya Congress na kumtaja kuwa muhalifu anayepaswa kuhukumiwa na hata kutaka aondolewe madarakani. Kwa msingi huo inatarajiwa kuwa kufikia wakati huo baadhi ya maseneta wa Republican watajiunga na wenzao wa Democrat na hivyo kufikia thuluthi mbili ya maseneta wanaohitajika kwa ajili ya kusaili na kumfuta kazi Trump.

Tags