Onyo la jeshi la Myanmar kwa wapinzani wa mapinduzi ya kijeshi
Jeshi la Myanmar limetoa onyo kali dhidi ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi ya kijeshi nchini humo ambao sasa wamekithirisha maandamano yao.
Tarehe Mosi ya mwezi huu wa Februari jeshi la Myanmar lilitangaza kudhibiti madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi nchini Myanmar, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo ambayo ilizua hofu ya kutokea mapinduzi. Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.
Taarifa ya jeshi la Myanmar iliyotangazwa kupitia televisheni na radio sambamba na kuwaonya wananchi wanaopinga mapinduzi hayo na ambao wamekuwa wakijitokeza na kuandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kwa siku kadhaa mtawalia, imewataka wasitishe maandamano hayo.
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Myanmar waliandamana Jumatatu ya juzi kwa siku ya tatu mtawalia katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, ambapo mbali na kulaani mapinduzi hayo waliwataka wanajeshi waliotwaa madaraka kwa nguvu kuwaachilia huru viongozi inayowashikilia kizuizini. Kuanza maandamano ya barabarani ya kulalamikia mapinduzi ya kijeshini nchini Myanmar na kuendelea maandamano hayo kwa siku kadhaa mtawalia, ni changamoto ambayo bila shaka jeshi lililopanga mapinduzi hayo liitibari.
Hata hivyo jeshi la Myanmar lilikuwa na matumaini kwamba, kisingizio ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge, ahadi yake ya kuitisha uchaguzi mwingine katika kipindi cha mwaka mmoja ujao na vilevile kukabidhi madaraka kwa serikali itakayopatikana kwa kura za wananchi, ni mambo ambayo yangekuwa na taathira na hivyo kupunguza malalamiko katika kipindi cha baada ya mapinduzi.
Kinyume na matarajio ya makamanda wa jeshi walioongoza mapinduzi ambao walikuwa walidhani kwamba, maandamano hayo yasingekuwa makubwa na yangeisha baada ya siku chache, hivi sasa maandamano hayo yamekuwa ni ya makumi ya maelfu ya watu na yamekuwa yakilaaani vikali ukiukaji wa demokrasia na kutumiwa kinyume cha sheria chombo cha jeshi na silaha kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali halali iliyochaguliwa na wananchi. Filihali inaonekana kuwa, changamoto inayowakabili wanajeshi wa Myanmar baada ya kutwaa madaraka ya nchi kinyamela, yumkini ikachukua mkondo mpana zaidi katika siku na majuma yajayo.
Endapo maandamano hayo yataendelea licha ya onyo la jeshi, basi wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Myanmar hawatakuwa na machaguo isipokuwa mawili tu ya kuondokana na changoto hiyo.
Chaguo la kwanza, ni kukandamiza maandamano hayo kwa mkono wa chuma, ambapo kutekeleza hili bila shaka kutapelekea kuuawa na kujeruhiwa waandamanaji. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, chaguo hilo litazidi kuitumbukiza Myanmar katika mgogoro mkubwa wa ndani na hata wanajeshi wanaoshika hatamu za nchi kuandamwa na mashinikizo ya kisiasa na pengine kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na asasi za kieneo na kimataifa.
Chaguo la pili ni wanajeshi kuandaa kifushi cha mapendekezo kwa viongozi wa waandamanaji na vyama vinavyopinga mapinduzi ili kuandaa mazingira ya kuwaridhisha na hivyo kuwafanya waachane na maandamano.
Ahadi ya jeshi la Myanmar ya kuitisha uchaguzi wa Bunge hapo mwakani na kukabidhi madaraka kwa serikali itayoundwa kutokana na matokeo ya uchaguzi huo, ni pendekezo ambalo wananchi wa nchi hiyo katu hawalikubali, na mahudhurio yao makubwa katika maandamano ya barabarani ni ishara ya wazi na na bayana ya kukataa mpango huo wa jeshi.
Kwa muktadha huo, ikiwa jeshi la Myanmar linataka kutuliza hali ya mambo linapaswa kuja na pendekezo jipya litakaloainisha hatima na mustakabali wa demokrasia baada ya mapinduzi ambapo moja ya hatua hizo bila shaka ni kupunguza muda liliotangaza wa mwaka mmoja wa kuitisha uchaguuzi mwingine wa Bunge na kuvishirikisha vyama vya siasa vya nchi hiyo katika mchakato huo.