UN: Somalia, Misri, Ethiopia zaongoza kwa ukeketaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i682-un_somalia_misri_ethiopia_zaongoza_kwa_ukeketaji
Umoja wa Mataifa umesema utamaduni wa kuwakeketa wasichana wadogo na wanawake umeongezeka kwa kiwango kikubwa katika nchi mbali mbali duniani, licha ya kampeni za kupiga vita jambo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2016 04:15 UTC
  • UN: Somalia, Misri, Ethiopia zaongoza kwa ukeketaji

Umoja wa Mataifa umesema utamaduni wa kuwakeketa wasichana wadogo na wanawake umeongezeka kwa kiwango kikubwa katika nchi mbali mbali duniani, licha ya kampeni za kupiga vita jambo hilo.

Ripoti mpya ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imeonyesha kuwa, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 walikeketwa kote duniani mwaka uliopita wa 2015, huku nusu ya idadi hiyo ikiwa ni katika nchi za Misri, Ethiopia na Indonesia. Hata hivyo Somalia inasalia kuwa nchi inayoongoza kwa ukeketaji duniani, ambapo 98% ya wanawake walio na umri wa kati ya miaka 15 na 49 wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika tayari wameshakeketwa. Kadhalika Guinea, Djibouti na Sierra Leone ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazoendeleza utamaduni huo. Geeta Rao Gupta, Naibu Mkurugenzi wa UNICEF amesema kuwa, takwimu hizo zinaashiria ongezeko la kesi milioni 70 za ukeketaji zilizoripotiwa mwaka 2014. Gupta amesema utamaduni huo unatofautiana katika kila nchi na jamii na kwamba baadhi ya jamii zinazotekeleza utamaduni huo zinayaweka maisha na mustakabali wa mtoto wa kike hatarini.

Uchunguzi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umebaini kuwa, asilimia kubwa ya jamii zinauenzi utamadauni huo kwa kuwa zinaufungamanisha na masuala ya kidini na sharti la kutekelezwa kabla ya ndoa.