Russia yaitaka Marekani iache kuiba rasilimali za Wasyria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Marekani inapaswa kukomesha tabia yake ya kuiba rasilimali za wananchi wa Syria, na badala yake ipambane na magenge ya kigaidi.
Sergei Lavrov amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, Moscow haidhani kuwa tishio la kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limeimarika kwa kiasi kikubwa katika nchi za Syria na Iraq.
Amesema Russia inazisaidia kihalali serikali za Syria na Iraq kusafisha mabaki ya wananchama wa Daesh, huku akizikosoa nchi ajinabi zilizozivamia nchi hizo za Kiarabu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amebainisha kuwa, Marekani na waitifaki wake katika muungano wa kijeshi eti wa kupambana na Daesh wanapaswa kulipa kipaumbele suala la kondoa tishio la magenge ya kigaidi kama ISIS na Hay'at Tahrir al-Sham, badala ya kukalia kwa mabavu sehemu kubwa za ardhi ya Syria na kuiba milki za taifa hilo.
Kwa miaka mingi sasa, wanajeshi vamizi wa Marekani wanaowahadaa walimwengu kuwa wanapambana na magenge ya kigaidi nchini Syria, wanashirikina na wapiganaji wa kundi la kigaidi la SDF katika kuiba ngano na mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mwezi Mei mwaka huu pekee, wanajeshi hao wa Marekani walipora malori 150 yaliyokuwa yamebeba ngano na magari zaidi ya 500 ya kubeba mafuta ya Syria na kuyapelekea kwenye kambi zao.