Oct 21, 2021 09:56 UTC
  • Wasiwasi wa taathira mbaya za vikwazo vya Marekani kwa afya ya wagonjwa wa Iran

Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran si tu kwamba vimeathiri uchumi wa nchi bali pia vimeathiri vibaya mfumo wa usambazaji dawa na vifaa vya tiba na afya nchini na hasa katika kipindi hiki kigumu cha kuenea duniani virusi hatari vya corona.

Katika uwanja huo Shirika la Afya Duniani WHO karibuni limetoa ripoti likisisitiza kwamba vikwazo hivyo dhidi ya Iran vimekiuka haki za binadamu za baadhi ya wagonjwa nchini. Ikiashiria baadhi ya matatizo wanayopitia baadhi ya wagonjwa wa Iran katika kujidhaminia dawa na vifaa vya matibabu kutokana na vikwazo vya Marekani, ripoti hiyo inasema vikwazo vya Marekai vimezuia wagonjwa hao kufikia baadhi ya haki zao za kibinadamu zikiwemo za kujidhaminia usalama wa maisha na afya.

Katika miaka ya karibuni Marekani imeongeza vikwazo vyake vya kadhlimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika nyanja tofauti zikiwemo za kisiasa na kiuchumi. Baada ya kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia yanayofahamika kama JCPOA viongozi wa Washington walizidisha maradufu vikwazo hivyo kwa ajili ya kuilazimisha Tehran isalimu amri na kutekeleza matakwa yao. Hata kama viongozi wa Iran katika kipindi hiki wamekuwa wakitekeleza siasa tofauti na kutegemea uwezo wa ndani ya nchi katika kukabiliana na vikwazo ili kudhamini baadhi ya mahitaji muhimu, lakini kuenea duniani virusi vya corona kumezidisha matatizo katika sekta ya matibabu na afya na hivyo kupunguza uwezo wa Iran wa kujidhaminia vifaa muhimu vinavyohitajika katika sekta hiyo. Hali hiyo pia imeathiri pakubwa wagonjwa wenye magonjwa sugu yasiyotibika kirahisi.

Shirika la Afya Duniani

Mahmoud Abbasi, Naibu Waziri wa Sheria wa Iran anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa ambaye pia ni Katibu wa Marejeo ya Kitaifa ya Azimio la Haki za Watoto anasema: Katika miaka michache iliyopita zaidi ya watoto 30 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi ya Epidermolysis Bullosa (EB) (wagonjwa wa kipepeo) walipoteza maisha kutokana na ukosefu wa upatikanaji dawa.

Taathira hasi za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran zimepeleka waathirika wa magonjwa sugu na maalumu wakabiliwe na matatizo makubwa katika kujidhaminia dawa za kupunguza makali ya magonjwa hayo. Kwa hakika vikwazo hivyo vimezuia kabisa kuingizwa nchini malighafi ya kutengenezea dawa na vifaa muhimu vya matibabu ya magonjwa sugu kama saratani. Kuenea corona duniani kumevuruga zaidi hali ya mambo katika uwanja huo.

Kuhusu suala hilo Said Namaki, Waziri wa zamani wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Udaktari wa Iran anasema: Vikwazo vya Kidhalimu vya Marekani na kuzuiwa taifa la Iran kujidhaminia dawa, vifaa vya matibabu na chakula ni tishio kubwa kwa afya ya Wairani na ni jinai dhidi ya binadamu.

Hii ni katika hali ambayo Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu linasisitiza kuwa ni dharura na haki ya watu wote kujidhaminia bidhaa za afya na maisha ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi, makazi na huduma za kimatibabu na kijamii.

Lakini pamoja na hayo, Marekani imekiuka sheria zote za kimataifa katika uwanja huo na kufunga njia zote za watu wa Iran kuweza kujidhaminia dawa na vifaa vya matibabu. Licha ya Marekani kudai kwamba bidhaa za dawa na matibabu haziko kwenye orodha ya vikwazo dhidi ya Iran lakini hatua za nchi hiyo za kubana, kutisha na kuzishinikiza benki zinazofanya miamala ya kifedha na Iran kuhusu suala hilo, kivitendo zimezuia uagizaji dawa na vifaa hivyo kuingia Iran.

Vikwazo vya dawa na bidhaa za matibabu vya Marekani dhidi ya Iran

Kuhusu hilo, Hussein Amir Abdollahiyan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema: Vikwazo hivyo ni ugaidi wa wazi dhidi ya watu wa Iran.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imekosoa vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Iran kutokana na kuwa vinakiuka wazi haki za binadamu za wagonjwa wa Iran katika hali ambayo Washington imeendelea kupuuza suala hilo na kuzidisha vikwazo na hivyo kuhatarisha zaidi maisha ya wagonjwa wanaokumbwa na maradhi sugu na yasiyo na tiba nchini.

 

Tags