Ukulima wa mipopi umeshamiri Afghanistan kutokana na vikwazo ilivyowekewa Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76728-ukulima_wa_mipopi_umeshamiri_afghanistan_kutokana_na_vikwazo_ilivyowekewa_taliban
Ukulima wa mipopi inayozalisha mihadarati ya kasumba umeongezeka nchini Afghanistan kutokana na vikwazo lilivyowekewa kundi la Taliban linalotawala nchi hiyo kwa sasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 10, 2021 02:40 UTC
  • Ukulima wa mipopi umeshamiri Afghanistan kutokana na vikwazo ilivyowekewa Taliban

Ukulima wa mipopi inayozalisha mihadarati ya kasumba umeongezeka nchini Afghanistan kutokana na vikwazo lilivyowekewa kundi la Taliban linalotawala nchi hiyo kwa sasa.

Shirika la habari la Sauti ya Afghani limeripoti kuwa, makadirio ya awali yanaonyesha kuwa, jumla ya hekta 224,000 za kilimo katika mikoa 22 ya Afghanistan zinatumika kwa ajili ya ulimaji wa mipopi.

Kutokana na Marekani kuzuia mali na mitaji ya Afghanistan iliyoko nchini humo kwa kisingizio cha kupinga Taliban kushika madaraka ya nchi, hali ambayo imesababisha kuongezeka umasikini nchini Afghanistan, watu wengi wameamua kujishughulisha na ukulima wa mipopi inayozalisha mihadarati ya kasumba ili kuweza kujikimu kimaisha.

Hata hivyo kukithiri ulimaji wa mipopi kumesababisha matatizo kadhaa yakiwemo ya biashara haramu ya magendo, uraibu wa madawa ya kulevya, uhalifu, kuvurugika uthabiti wa kijamii, kudhoofika hali za afya za watu na kuharibika muundo wa kiuchumi wa Afghanistan.

Imran Khan

Hayo yanaripotiwa huku Waziri Mkuu wa Pakistan akizidi kuihimiza jamii ya kimataifa ichukue hatua ya kuisaidia Afghanistan ili kuipeusha na janga la maafa ya kibinadamu.

Imran Khan ameashiria indhari iliyotolewa karibuni na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) kuhusu hatari ya kutokea hali mbaya ya kibinadamu nchini Afghanistan na akasema, kile alichotahadharisha yeye hapo kabla kinatiliwa mkazo sasa na mkuu wa WFP.

Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, asilimia 95 ya Waafghani hawana chakula cha kutosha na inahofiwa kuwa watu milioni 23 nchini humo watakabiliwa na hatari ya baa la njaa.../