Dec 04, 2021 02:39 UTC
  • Ufaransa yapinga ombi la Uingereza, mizozo yashadidi baina ya pande mbili

Baada ya siku saba, Ufaransa imekataa ombi la Uingereza lililokuwa limetolewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Boris Johnson kwa Rais Emmanuel Macron.

Hii ni licha ya kwamba, kwa mujibu wa kaida za kisiasa na kidiplomasia, barua ya Boris Johnson ilipaswa kujibiwa na Macron lakini kinyume chake, barua hiyo imejibiwa na Waziri Mkuu wa Ufaransa, Jean Castex ambaye amekataa pendekezo la Johnson la kufanya doria ya pamoja katika maji ya Ufaransa kwa shabaha ya kuzuia wahajiri wanaoelekea Uingereza. 

Castex ameandika kuwa: "Tumekataa baadhi ya mapendekezo ya Uingereza. Kwa mfano hatuwezi kukubali polisi au wanajeshi wa Uingereza wafanye doria katika pwani yetu; hii ni haki yetu ya kimamlaka."

Jean Castex

Inaonekana kuwa, uhusiano wa nchi hizo mbili kubwa za Ulaya umeingia katika awamu mpya ya mizozo na mivutano ya pande mbili. Baada ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit), Paris na London zimekuwa na hitilafu kuhusiana na masuala mengi ikiwa ni pamoja na haki ya uvuvi katika Mfereji wa Manchi, hali ya Ireland ya Kaskazini, ushirikiano wa nchi tatu za Marekani Australia na Uingereza katika uundaji wa nyambizi ya nyuklia katika kalibu ya makubaliano ya AUKUS na kutengwa Ufaransa katika muungano huo, wimbi la wahajiri kuelekea Uingereza kupitia Ufaransa na mustakbali wa uhusiano wa kibiashara wa pande mbili. Kwa sasa nchi hizo mbili ziko kwenye mzozo kuhusu harakati kubwa ya wahajiri wanaotafuta hifadhi wanaotokea pwani ya kaskazini mwa Ufaransa wakielekea pwani ya kusini mwa Uingereza kwa kutumia vyombo visivyo salama kupitia Mfereji wa Manch. Baada ya wakimbizi wasiopungua 27 kuzama baharini katika Mfereji wa Manch kufuatia kupinduka kwa boti iliyokuwa imewabeba, serikali zote mbili za Ufaransa na Uingereza zilijaribu kujivua lawama za maafa hayo ya binadamu na kutumia janga hilo kisiasa.

Ukweli ni kwamba, Mfereji wa Manch na matukio yanayoambatana na majaribio ya wakimbizi kuelekea pwani ya Uingereza kupitia njia hii ya majini daima yamekuwa yakizusha mizozo na mivutano kati ya Paris na London. Maafisa wa serikali ya kihafidhina ya Uingereza wanasema juhudi za Ufaransa za kudhibiti mgogoro wa wahajiri katika eneo hilo hazitoshi. Wakati huo huo, maafisa wa Paris wameikosoa London kwa kutotekeleza ahadi yake ya msaada wa kifedha kwa Ufaransa ili kuzuia wimbi la wahajiri wanaotaka kuvuka Mfereji wa Manch kuelekea Uingereza. Bella Sankey ambaye ni mkuu wa kundi la watetezi wa haki za wakimbizi wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza anasema: "Uingereza na Ufaransa hazina irada na azma ya kisiasa ya kutatua mzozo wa wahamiaji na wakimbizi katika Mfereji wa Manch. Vifo vya hivi majuzi vya wahamiaji katika mfereji huo vilitabirika na kulikuwepo uwezekano wa kuepukika. Kwa bahati mbaya, tuna serikali nchini Uingereza ambayo inaendeleza kikamilifu sera iliyoshindwa ya kuwafukuza watu wanaotafuta hifadhi nchini, bila kujali matokeo."

Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson hivi karibuni alichapisha barua yake kwa Rais wa Ufaransa kwenye mtandao wa Twitter kwa shabaha ya kuiwekea mashinikizo zaidi Paris na kurusha mpira kwenye ardhi ya Ufaransa. Mkabala wake, jibu la Rais Emmanuel Macron kwa barua ya Johnson pia halijawahi kushuhudiwa. Akiwa katika mji mkuu wa Croatia, Zagreb, Macron aliwaambia washauri wake kwamba Boris Johnson, mara zote, amekuwa akianzisha mchezo wa sarakasi badala ya kufanya mazungumzo ya busara, na kwamba inasikitisha kuona nchi kubwa (Uingereza) ikiongozwa na damisi.

Boris Johnson na Macron

Suala hili limewakasirisha sana viongozi wa London. George Freeman ambaye ni mjumbe katika Baraza la Mawaziri la Uingereza, amesema: "Matamshi ya Rais wa Ufaransa kuhusu Boris Johnson "hayasaidii" na yametukatisha tamaa' vilevile Waziri Mkuu wetu sio chale."

Haya yote yanaonesha kuwa, mvutano kati ya Ufaransa na Uingereza sasa umefikia kiwango cha viongozi wa nchi hizo mbili, na tunaweza kutabiriwa kuwa, mzozo na hitilafu za Paris na London utapanuka na kushadidi zaidi. 

Tags