Kuongezeka indhari kuhusu uwezekano wa kutokea vita mashariki mwa Ulaya
(last modified Sat, 12 Feb 2022 10:13:24 GMT )
Feb 12, 2022 10:13 UTC
  • Kuongezeka indhari kuhusu uwezekano wa kutokea vita mashariki mwa Ulaya

Nchi za Magharibi zinaendelea kutoa tahadhari mbalimbali kuhusu uwezekano wa Russia kuishambulia Ukraine kufuatia kuongezeka mivutano huko Ulaya Mashariki kati ya Moscow na Kiev.

Kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetoa taarifa na kutangaza kuwa Lloyd Ashton Waziri wa Ulinzi wa Marekani amezungumza kwa njia ya simu na wenzake wa Poland, Ujerumani, Canada, Ufaransa, Romania na Italia na kutahadharisha kuwa  Russia inaweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine  wakati wowote kuanzia sasa.  

Antony Blinken Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani pia jana Ijumaa alidai kuwa Russia inakusanya wanajeshi zaidi katika mpaka wa Ukraine. Aidha alidai kuwa hujuma hiyo ya Russia huenda ikajiri katika michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi huko Beijing. Wakat huohuo katika kuendelea madai hayo ya viongozi wa Magharibi, Katibu Mkuu wa Muungano wa Nato Jens Stoltenberg amesisitiza juu ya hatari ya kujiri vita dhidi ya Ukraine na kusema nchi za Ulaya zinapasa kujiandaa kwa wakati mbaya zaidi. Stoltenberg amesisitiza kuwa, muda wa kutolewa indhari kuhusu uwezekano wa kujiri mashambulizi umekwisha. Amesema Nato haitajadili na kufikia muafaka kuhusu kanuni na sheria zake ikiwemo suala la kuchagua waitifaki wa muungano huo. 

Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Nato 

Baadhi ya viongozi wa Magharibi wametoa wito wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Ukraine kwa njia za kidiplomasia katika hali ambayo Marekani, Uingereza na nchi nyingine wanachama wa muungano wa Nato wiki iliyopita zilituma maelfu ya wanajeshi wao katika nchi zilizo karibu na Russia. Karibu wanajeshi elfu tatu wa Marekani wametumwa  Poland na Romania katika kile kilichotajwa kuwa kwa lengo la kuimarisha kambi ya mashariki ya Nato. Wakati huo huo Pentagon imetangaza kuwa Lloyd Ashton Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameamuru askari wengine elfu tatu vya nchi hiyo wawe wameelekea Poland katika muda wa siku mbili huku Washington ikituma pia ndege za kivita aina  ya F-16 huko Romania. 

Llyod Ashton, Waziri wa Ulinzi wa Marekani 

Vyombo vya habari vya Magharibi pia vimekwenda mbali zaidi ambapo shirika la habari la Bloomberg la nchini Marekani limedai kuwa upo uwezekano wa Russia kuishambulia Ukraine na kwamba mashambulizi yataanza siku ya Jumanne. Wakati huohuo kuongezeka propaganda za uwezekano wa Russia kutekeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine kumezipelekea akthari ya nchi za Magharibi kutaka kuwaondoa raia wao huko Ukraine na hata shirika la habari la Associated Press Jumamosi hii limewanukuu viongozi wa Washington wakisema kuwa Rais Joe Biden ana mpango wa kuufunga ubalozi wa nchi hiyo huko Ukraine. 

Inaonekana kuwa Marekani na Nato zinachukua hatua mpya ili kufanikisha lengo lao kuu na la muda mrefu yaani kuzidisha uwepo wa vikosi vyao, zana za kijeshi na pia taasisi ya Nato kandokando ya mipaka ya Russia kwa kisingizio kwamba kuna uwezekano Russia ikaishambulia Ukraine. Hatua hizo za Marekani na Nato zitaichochea Moscow nayo kuchuka hatua za kulipiza kisasi; jambo litalokoleza moto na kushadidisha mivutano na uwezekano wa kutokea mapigano mashariki mwa Ulaya.

Moscow hivi karibuni ilizitaka Marekani na Nato zijitoe katika mpango wa kuiunganisha Ukraine katika muungano wa Nato katika kalibu ya mapendekezo mapya  na kuacha kutuma wanajeshi wao katika nchi za mashariki mwa Ulaya na kwamba nchi hizo zipunguze wanajeshi wake barani Ulaya. Pamoja na hayo, Russia ambayo imewalisha maombi yake hayo katika fremu ya kulinda usalama wake wa taifa mkabala wa hatua za uvamizi na  kichokozi za Nato khususan sera za kujipanua kuelekea upande wa mashariki, imekabiliwa na jibu hasi la Washington na muungano wa Nato. 

Ukweli ni kuwa, nchi za Magharibi huku zikiongozwa na Marekani zinahusika pakubwa na hali mbaya ya usalama huko mashariki mwa Ulaya khususan hali ya hatari inayoshuhudiwa katika mipaka ya Russia na Ukraine. Hakuna shaka kuwa Kremlin nayo haitapuuza kutozingatia nchi za Magharibi matakwa yake ya kiusalama; na itatoa jibu kwa hatua hiyo na khususan kuhusu kadhia ya Ukraine. Taaban Russia mara kadhaa imetamka wazi kuwa haina mpango wa kuishambulia Ukraine. 

Vladimir Isachenkov mwandishi habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Mlango wa diplomasia katika mgogoro huo utafungwa kwa kuzingatia hatua ya Russia kujizatiti kijeshi karibu na Ukraine huku Magharibi nayo ikipinga pakubwa matakwa ya kiusalama ya Moscow.