Vita vya Ukraine na mabadiliko ya uwiano wa nguvu barani Ulaya
Kuanza vita vya Russia na Ukraine kumevuruga mlingano wa kijeshi hasa miongoni mwa mataifa ya Ulaya, kiasi kwamba Ujerumani imetenga Euro bilioni 100 kwa ajili ya bajeti yake ya kijeshi, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko ya mfumo wake wa ulinzi.
Akibainisha kuwa Ujerumani inapaswa kuwekeza katika usalama wake na pia katika kulinda uhuru na demokrasia, Kansela Olaf Schultz wa Ujerumani amesema: "Hii ina maana kwamba Ujerumani inatumia asilimia mbili ya pato lake la taifa kushughulikia masuala ya ulinzi."
Mabadiliko haya ya kimkakati yanakuja wakati ambapo Ulaya, haswa Ujerumani, katika miaka ya karibuni imekuwa ikitekeleza hatua za kujilinda tu na hata kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel miaka michache iliyopita alikataa kuongeza bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo kwa asilimia 2% ya pato la taifa. Kuzuka vita huko Ukraine, kumeipelekea Ujerumani ifanye mabadiliko makubwa katika sera zake za ulinzi na kijeshi ambapo sasa inatekeleza hatua za kuimarisha na kubadilisha sera hizo na kuzifanya kuwa za hujuma.
Sio Ujerumani pekee bali nchi karibu zote za Ulaya sasa zinatumia mbinu hiyo. Katika uwanja huo, Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema: "Tunatuma silaha kusaidia jeshi la Ukraine katika vita hivi, kwa sababu tuko katika hali ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma."
Umoja wa Ulaya ambao katika miongo ya karibuni umekuwa ukiimba kauli mbiu ya umoja na mshikamano, katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukisisitiza kuimarishwa vikosi vya kijeshi vya umoja huo mbali na shirika la kijeshi la NATO na kuundwa kikosi kimoja cha kijeshi cha Ulaya bila ya kushirikishwa Marekani. Takwimu za Shirika la Ulinzi la Ulaya zinaonyesha kuwa mwaka 2020 nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilitumia Euro bilioni 198 kwa ajili ya masuala ya kijeshi, licha ya uwepo wa janga la corona.
Ulaya sasa imebadili mtazamo wake na kuimarisha silaha zake na wakati huo huo, kutuma silaha za kisasa kwa ajili ya kuisaidia Ukraine, ikiwa ni pamoja na makombora ya kutungulia ndege za kivita. Kansela Schultz wa Ujerumani amesema kuhusu vita vinavyoendelea huko Ukraine kwamba: "Jukumu letu ni kuisaidia Ukraine kujilinda dhidi ya jeshi la Putin." Mbali na Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Poland, Slovakia, Estonia, Latvia, Ubelgiji na Jamhuri ya Czech pia zimetangaza kutuma zana za kijeshi huko Ukraine. Kwa mujibu wa ripoti za karibuni, misaada ya nchi za Ulaya kwa Ukraine ni pamoja na mafuta, bunduki, silaha za kukabiliana na vifaru na makombora ya Stinger.
Wakati huo huo, Russia imejibu uchochezi wa Ujerumani katika uwanja huo ambapo ubalozi wake mjini Cairo umesema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Russia ingali inakumbuka vizuri jinsi silaha za Ujerumani ziliwaua Warussia. Ujerumani sasa inaonekana kuingia katika awamu ya tatu ya utawala wa Hitler, kwa kutaka kuwasaidia Wanazi mamboleo wa Ukraine kufanya vivyo hivyo."
Hali hiyo imeipelekea Belarus ambayo, wakati mmoja ikiwa chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani, ililazimika kuharibu silaha zake za nyuklia kufuatia kusambaratika Muungano wa Kisovieti, nayo izionye nchi za Magharibi kuhusu uwezekano wa kuwekwa makombora ya nyuklia katika ardhi yake. Kufanyika kura ya maoni kwa ajili ya kurekebisha katiba kuhusu uwekaji silaha za nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo ni moja ya hatua za kivitendo zilizochukuliwa katika uwanja huo.
Kuhusu suala hilo, Rais Alexander Lukashenko wa Belarus amesema: "Iwapo tishio la nchi za Magharibi litatekelezwa, Belarus itakuwa mwenyeji wa silaha za nyuklia za Russia, na inaweza kupokea silaha za nyuklia ikiwa washindani na wapinzani wake watachukua hatua za kipumbavu na zisizo za busara."
Ni wazi kuwa sera za kijeshi za nchi za Ulaya zimebadilika kimsingi, na kama ilivyokuwa kabla ya Vita Vikuu vya II vya Dunia nchi hizo sasa zimechukua mwendo-kasi wa kujirundikia silaha za kisasa na kuingia kwenye mshindano ya silaha ambayo bila shaka yanahatarisha usalama na amani ya dunia.