Apr 19, 2022 10:55 UTC
  • Iran yalaani kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu nchini Uswidi

Ali Bahadori Jahromi, Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ukurasa wake binafsi wa kijamii akijibu vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya hususan nchini Uswidi kwamba: “Uhuru wa kidini umebadilishwa kuwa kukashifiwa dini za mbinguni, na uhuru wa kujieleza umekuwa chombo cha kueneza misimamo mikali na ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi."

Ameendelea kusema: "Matusi ya aibu dhidi ya Waislamu bilioni 2 tena katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa uungaji mkono rasmi wa polisi, sio suala la haki za binadamu, bali ni chuki na hatua iliyo dhidi ya maisha ya kiroho ya wanadamu."

Matamshi hayo ya Bahadori Jahromi yanaashiria hatua mpya za mabavu na ugaidi ambao umekuwa ukitekelezwa na magenge yenye misimamo mikali ya kupindukia mpaka huko Uswidi dhidi ya Uislamu na Waislamu, kwa uungaji mkono wa wazi wa polisi ya nchi hiyo. Uingiliaji kati wa polisi ambao walitumia mabavu katika kukabiliana na maandamano ya Waislamu waliokuwa wanalalamikia kuivunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika mji wa Norrkoping Uswidi, Jumapili iliyopita, ulipelekea watu watatu kujeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi na polisi hao.

Machafuko katika miji kadhaa ya Uswidi yalianza Alhamisi kufuatia vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu ambavyo vilitekelezwa na makundi ya nchi hiyo yenye misimamo ya kupindukia mipaka, ambapo polisi waliingilia kati kwa maslahi ya makundi hayo. Rasmus Paludan, kiongozi wa chama chenye mielekeo mikali ya mrengo wa kulia cha "Hard Line" na ambaye ana uraia wa nchi mbili za Denmark na Uswidi, anapanga na kutekeleza hatua kadhaa za chuki dhidi ya Uislamu na wahamiaji nchini , moja ya hatua hizo ikiwa ni kuchoma moto hadharani Qur'ani Tukufu, kama ishara ya kuonyesha chuki dhidi ya Uislamu na kupinga uwepo wa Waislamu barani Ulaya.

Malalamiko dhidi ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi

Hata hivyo, jaribio la hivi karibuni la Rasmussen na wafuasi wake wengine wenye siasa za chuki kali wa mrengo wa kulia lilishindwa siku ya Alhamisi kutokana na kuenea maandamano ya Waislamu katika mji wa Linkoping ulioko mashariki mwa Uswidi. Hilo halikuwa jaribio la kwanza la kundi hilo la mrengo wa kulia katika uwanja huo. Mnamo Agosti 28, 2020, mapigano kama hayo pia yalitokea katika mji wa Malmo nchini Uswidi, na kusababisha ghasia na vurugu za mitaani. Katika tukio hilo wananchama wa chama cha Hard Line mbali na kupiga nara dhidi ya Uislamu, walichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu ambapo mamia kadhaa ya Waislamu wakazi wa Malmo waliandamana kulaani vikali kitendo hicho cha chuki na uvunjiwaji heshima matukufu ya Kiislamu. Rasmus Paludan, kiongozi wa chama cha Hard Line, ambacho wanachama wake wana historia ya kuchoma Qur'ani huko Copenhagen, mji mkuu wa Denmark, alisema wakati huo kwamba lengo lake ni 'kuwaamsha watu wa Uswidi.'

Kisingizio kinachotumiwa na serikali za Denmark na Uswidi katika kukipa chama cha Paludan na wafuasi wenye misimamo ya kupindukia mipaka kibali cha kuyavunjia heshima matukufu ya Uislamu na kuumiza hisia za Waislamu kwa kuwachomea moto kitabu chao kitakatifu cha Qur'ani, ni eti kutetea uhuru wa kusema. Hii ni katika hali ambayo vipimo vya kindumakuwili vinavyotumiwa na nchi za Magharibi na hasa za Uaya kuhusiana na suala zima la uhuru wa kujieleza vinathibitisha wazi kuwa suala hilo hupewa umuhimu pale tu masuala yanayolengwa na Wamagharibi, kama vile chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na kuvunjiwa heshima matukufu yao yanapohusika. La sivyo, kupinga mambo kama vile holocaust, yaani madai ya kuuawa Mayahudi katika Vita vya Pili vya Dunia au kuitetea Russia kuhusu vita vinavyoendelea huko Ukraine hukabiliwa na hatua kali za Ulaya na hata wahusika kufuatiliwa kisheria au kuwekewa vikwazo mbali mbali.

Sehemu ya maandamo ya kupinga Qur'ani kuvunjiwa heshima

Iran imelaani mara nyingi siasa hizo mbovu na za undumakuwili za serikali za Magharibi zikiwemo za Ulaya kuhusiana na suala la uhuru wa kujieleza ambapo vitendo vinavyovunjia heshima matukufu ya Kiislamu huruhiswa kuendelea na hata kuungwa mkono katika nchi hizo. Kuhusu suala hilo Muhammad Swadeq Khiyatiyan, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratijia katika Ofisi ya Rais wa Iran anasema: Katika ulimwengu ambao kwa misingi ya kisiasa na kibaguzi, vyombo vya habari na watafiti hata hawana ruhusa ya kukaribia baadhi ya mambo maalumu, kuhalalisha kitendo kiovu cha kuchoma moto Qur'ani kwa kisingizio cha eti 'uhuru wa kijieleza' ni kutusi na kudharau hisia za walengwa (wasikilizaji na watazamaji). Kile ambacho kimetendeka kwa uhuru kamili huko Uswidi na pia kupitishwa katika sheria za serikali na vyombo vya usalama na hasa polisi ya nchi hiyo, sio uhuru wa kujieleza bali ni mfano halisi wa kueneza chuki na ubaguzi, jambo ambalo bila shaka linaenda kinyume na misingi ya maadili, mantiki, thamani za demokrasia na haki za binadamu. Wale wanaounga mkono hatua hizo za kichochezi wanapasa pia kubeba dhima ya matokeo yake.

Tags