May 22, 2022 02:57 UTC
  • Mabadiliko katika Baraza la Mawaziri la Macron, marekebisho yanayolenga kutafuta kukubalika na umma

Mwezi mmoja baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa Emmanuel Macron Rais wa nchi hiyo akiwa na lengo la kutafuta uungaji mkono na kuwaridhisha wapigakura na hivyo serikalii yake iungwe mkono zaidi, amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri.

Ijumaa iliyopita, Macron alitangaza kufanya mabadiliko katika serikali yake ambapo amewabadilisha mawaziri wa wizara mbili nyeti za Mashauri ya Kigeni na Ulinzi.

Catherine Colonna, balozi wa zamani wa Ufaransa nchini Uingereza ameteuliwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa na kurithi mikoba ya Jean-Yves Le Drian. Sebastien Lecornu, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Mipaka ya Baharini ameteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Ulinzi akichukua nafasi ya Florence Parly ambaye ameondolewa katika wadhifa huo. Mawaziri wa Mambo ya Ndani, Uchumi na Mahakama wamebakishwa katika nafasi zao. Aidha Pap Ndiaye mtaalamu wa masuala ya ukoloni na mahusiano ya mbari, ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Malezi. Kadhalika Agnes Pannier-Runacher, ameondolewa katika Wizara ya Viwanda na kupekwa katika Wizara ya Nishati.

Siku chache zilizopita, Rais Emmanuel Macron alianza kufanya mageuzi katika baraza lake jipya la mawaziri baada ya kumteua Bi Elisabeth Borne kuwa Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa. Hii ni mara ya kwanza nchini Ufaransa kwa mwanamke kuwa Waziri Mkuu katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.

Emmanuel Macron Rais wa Ufaransa ambaye anakabiliwa na changamoto nyingi katika duuru ya pili ya uongozii wake

 

Emmanuel Macron aliibuka na ushindi wa asilimia 58 katika uchaguzi wa mwezi Aprili mwaka huu mkabala na asilimia 42 ya mpinzani wake mkuu na mkongwe Marine Le Pen, kimsingi kiongozi huyo ni mwakilishi wa asilimia 38 tu ya wananchi wa Ufaransa waliotimiza masharti ya kupiga kura na mwakilishi wa asimilia 27 ya wananchi wa nchi hiyo ya bara Ulaya.

Licha ya kuapishwa kwake kuhudumu kwa muhula wa pili wa miaka mitano, Rais Marcon anakabiliwa na changamoto za ndani na nje ya nchi ambazo anatarajiwa kupambana nazo.

Baadhi ya changamoto anazokabiliwa nazo ni pamoja na kutekeleza mageuzi aliyoahidi kufanya wakati akichaguliwa kwa awamu ya kwanza mwaka wa 2017 akiwa rais mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuchaguliwa kuongoza Ufaransa.

Kwa kuzingatia uchaguzi wa mwezi uliopita, Macron amedai kuwa, ni mwanasiasa mwenye misimamo ya wastani ambaye anataka kuiongoza Ufaransa kwa mbinu tofauti kabisa na uongozi wake wa duru ya kwanza na kwamba, atajikita zaidi katika suala la kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Macron mwenyewe amekiri kwamba, sehemu ya kura alizopata katika duru ya pili ya uchaguzi huo alipigiwa na wapiga kura ambao nia yao ilikuwa ni kuzuia Marine Le Pen asishinde kiti hicho.

Maandamano Ufaransa

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Wafaransa walikuwa na machaguo mawili ambayo ni baya na baya zaidi, hivyo hawakuwa na budi ghairi ya kuchagua chaguo baya mbele ya chaguo baya zaidi. Jean-Luc Melenchon, mmoja wa wanasiasa wa mrengo wa kushoto ambaye alishika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais alisema katika radiamali yake kwa ushindi wa Macron kwamba, Macron ni rais mbaya kabisa wa tano wa Ufaransa ambaye ameogelea katika bahari ya kura za kujizuia, nyeupe na batili.

Kwa kuzingatia mdororo wa uchumi uliosababishwa na msambao wa virusi vya Corona na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia kutokana na vita vya Ukraine, filihali Macron anapaswa kuwakinaisha wapiga kura kwamba, mpaka wakati wa kufanyika uchaguzi wa Bunge mwezi Juni mwaka huu, atakuwa amezingatia matakwa yao.

Tags