Sep 12, 2022 07:02 UTC
  • Ugiriki: Vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia vimetudhuru wenyewe

Waziri Mkuu wa Ugiriki amesema kuwa, vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow vimetoa pigo la kiuchumi kwa nchi zenyewe za Ulaya kabla ya hata Russia.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Kyriakos Mitsotakis akisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, nchi za Magharibi zimekumbwa na madhara mengi kwa hatua yao ya kuiwekea vikwazo Russia na ingawa zinakiri lakini haziko tayari kubadilisha siasa zao hizo.

Amesema, vikwazo dhidi ya Russia vimetoa pigo kwa uchumi wa nchi zenyewe za Ulaya na iwapo nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hazitotafuta njia za kusimisha vita vya Ukraine, hali itazidi kuwa mbaya. 

Matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Ugiriki yametolewa katika hali ambayo miji kadhaa ya nchi za Ulaya imeshuhudia maandamano ya kulalamikia ongezeko la bei za nishati, huku mgogoro wa mafuta ya petroli na gesi ukiendelea kuyasumbua mataifa mengi ya bara Ulaya.

Ulaya imeiwekea Russia vikwazo, sasa maandamano ya kulalamikia nishati yaikumba miji ya Ulaya kwenyewe

 

Maandamano makubwa ya Vizibao vya Njano yameshuhudiwa nchini Ufaransa, kulaani kupanda kwa bei za nishati katika nchi hiyo ya Ulaya.

Aidha maandamano kama hayo yameshuhudiwa katika mji mkuu wa Vienna, Austria na pia katika mji wa Naples nchini Italia. Habari zaidi zinasema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Luigi Di Maio ameshambuliwa na waandamanaji waliokuwa na hasira na kumtaja kuwa 'msaliti'.

Waandamanaji jijini Vienna wamesikika wakipiga nara dhidi ya Umoja wa Ulaya, shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, Chansela wa nchi hiyo, Alexander Schallenberg na mabwenyewe wanaofaidika na vita vya Ukraine.

Tags