Bin Salman akaribishwa kwa maandamano nchini Uingereza
Makumi ya watetezi wa haki za binadamu wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini London, kulaani safari ya Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman nchini Uingereza.
Wananchi wa Uingereza pamoja na wakosoaji wa Saudia walioko London wameshiriki maandamano hayo ya kukosoa safari ya Bin Salman nchini humo, ambaye wanasema rekodi nyeusi ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa "Susia makatili" na "Achana na Yemen" wakiitaka serikali ya Riyadh isitishe mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya wananchi wa Yemen ya tangu mwaka 2015.
Aidha safari hiyo imekosolewa na duru za haki za binadamu kwa London kupuuza nafasi ya Bin Salman katika mauaji ya mwanahabari mkosoaji Jamal Khashoggi mwaka 2018 katika ubalozi mdogo wa Saudia nchini Uturuki.
Bin Salman yuko London kushiriki mazishi ya Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza. Ikumbukwe kuwa, Malkia huyo ambaye ameitawala nchi hiyo ya Ulaya kinyume na demokrasia kwa muda wa miaka 70 kuanzia mwaka 1952 hadi 2022, alifariki dunia Alkhamisi ya wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 96.
Stephen Bell, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Tuko hapa kupinga safari ya Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman nchini Uingereza. Anadai amekuja kumuomboleza Malkia, lakini akiwa hapa, ni nani atakayewaomboleza Wayemen 377,000 waliokufa kutokana na vita vyake dhidi ya taifa la Yemen?
Bell ameutaja utawala wa Aal-Saud kuwa wa kidikteta, kwa kuwakamata kinyume cha sheria na kuwanyonga wafungwa wa kisiasa na wakosoaji wa utawala huo wa kifamilia.