Nchi za Magharibi zashindwa kuitenga Russia
Kufuatia kuzorota hali ya uchumi na usalama barani Ulaya, tofauti za mitazamo kuhusu sera za nje na usalama wa bara Ulaya zimeongezeka, hasa kuhusiana na suala la Russia. Huku viongozi wa Ulaya wakizungumzia siasa za kuitenga Russia, baadhi ya wanasiasa wa bara hilo wanaonya dhidi ya kukatwa kabisa uhusiano na nchi hiyo.
Katika uwanja huo Angela Merkel, mwanasiasa mkongwe na kansela wa zamani wa Ujerumani ameonya dhidi ya suala hilo na kusisitiza kuwa amani ya kudumu itapatikana tu barani Ulaya kwa ushirikiano wa Moscow.
Kufuatia vita vya Russia na Ukraine ambavyo vilisababishwa na msimamo wa Kiev kung'ang'ania kupewa uanachama katika jumuiya ya kijeshi ya nchi za Magharibi NATO na licha ya maonyo ya Moscow, Wamagharibi waliingia vitani kuiunga mkono nchi hiyo na kutekeleza siasa za adhabu na vikwazo dhidi ya Moscow. Kwa hakika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetayarisha na kutekeleza vifurushi kadhaa vya vikwazo dhidi ya Russia, vikiwemo vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta na gesi ya Russia, vikwazo ambavyo kabla ya kuiadhibu Russia, vimedhuru uchumi wa nchi hizo zenyewe. Hivi sasa uchumi wa nchi nyingi za Ulaya umeharibika kiasi kwamba watu wa nchi hizo wanalalamika na kuzikosoa vikali serikali zao kutokana hali mbaya ya uchumi inayowakabili.
Ongezeko la maandamano ya wafanyakazi nchini Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na maonyo mfululizo yanayotolewa kuhusu majira yajayo ya baridi kali na uhaba wa mafuta na nishati, yote hayo yanatathminiwa katika uwanja huo. Siku chache zilizopita, mamia ya waandamanaji wa Ujerumani walikusanyika mbele ya "Bundestag" (bunge la nchi hiyo) na kutaka kufutwa vikwazo vya nchi za Magharibi, ikiwemo Ujerumani, dhidi ya Russia. Waandamanaji huko Vienna, mji mkuu wa Austria, pia wametaka kupunguzwa bei ya bidhaa, kuondolewa vikwazo dhidi ya Russia na kuimarishwa uhusiano na Moscow. Mjini Roma, mji mkuu wa Italia, pia vyama vya wafanyakazi vimefanya maandamano dhidi ya ongezeko la bei za bidhaa, ughali wa maisha na ushuru wa nishati.
Licha ya machafuko yote yanayozikumba nchi za Ulaya, lakini bado nchi hizo zinaendelea kutoa misaada ya silaha na fedha kwa Ukraine ili kuishinikiza Russia, jambo ambalo limeipelekea Moscow kutoa tahadhari na kuonya kuwa kutumwa silaha za nchi za Magharibi nchini Ukraine ndiko kunarefusha muda wa vita nchini humo.
Uingiliaji huo unaoongezeka kila siku wa nchi za Magharibi huko Ukraine umempelekea Rais Vladimir Putin wa Russia kuonya kuhusu uwezekano wa kutumika silaha za nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo. Amesema iwapo usalama wa ardhi ya Russia utahatarishwa, Moscow haitasita kutumia "zana zote zilizopo" kwa ajili ya kuilinda Russia.
Suala la uwezekano wa kutumika silaha za nyuklia nchini Ukraine sasa linapewa uzito na nchi za Magharibi, kiasi kwamba baadhi ya viongozi wa nchi hizo wamechukulia onyo hilo la Putin kuwa onyo zito na la kweli.
Akiashiria maneno ya rais wa Russia, Merkel amesisitiza: Walimwengu hawapaswi kupuuza maneno ya Putin ambayo yanaonyesha ukomavu na busara ya kisiasa, bila kuyatathmini vizuri na kuyachukulia tu kuwa ni ya kipuuzi. Ushirikiano wa nchi za Magharibi na Putin unaweza kusaidia kutuliza hali ya mambo.
Mvutano kati ya Ulaya na Russia umeongezeka kufuatia kura ya maoni iliyopelekea kuunganishwa maeneo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhia na Russia. Marekani na nchi nyingine za Magharibi zilipinga vikali suala hilo na kuzidisha vikwazo dhidi ya Mosscow. Kufuatia mvutano huo unaoongezeka kila siku, baadhi ya viongozi wa Ulaya wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na mustakbali wa bara hilo. Viongozi kama vile Rais Katalin Novak wa Hungary ambaye amekosoa na kukataa kufuata siasa za Ulaya kuhusu Russia amesema: Vikwazo dhidi ya Russia vimeathiri nchi zote za Ulaya kwa sababu bei za bidhaa na ughali wa maisha unaendelea kuongezeka.
Kwa kweli, itakuwa vigumu sana, iwapo haitawezekana kabisa, kwa bara Ulaya kushuhudia utulivu wa kijamii na kiuchumi bila kushirikiana na Russia, na kama alivyosema Angela Merkel, amani ya kudumu barani Ulaya itapatikana tu kwa ushiriki wa Russia.