Feb 13, 2023 02:34 UTC
  • Polisi ya Ufaransa yakandamiza maandamano ya wananchi

Askari polisi nchini Ufaransa wamewashambulia vibaya mamia ya maelfu ya watu walioshiriki maandamano ya kulalamikia sera za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo, na hususan mageuzi tata ya pensheni yaliyotazamiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu wa 2023.

Polisi ya Ufaransa imewashambulia waandamanaji hao kwa mabomu ya gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira. Makumi ya waandamanaji hao wamejeruhiwa, baadhi yao wakilazwa hospitalini kwa majeraha.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, takriban watu milioni moja wameshiriki kwenye maandamano hayo ya mwisho wa wiki katika miji mbali mbali ya nchi hiyo ikiwemo Paris, Nice, Marseille, Toulouse, na Nantes.

Hatua hizo za ukandamizaji za polisi wa Ufaransa dhidi ya waandamanaji wanaopinga mfumo wa kibepari, zimekabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mbali na kulalamikia mageuzi hayo ya sheria ya kustaafu, waandamanaji hao nchini Ufaransa wanalalamikia pia mfumko wa bei za bidhaa, mgogoro wa nishati, na ughali wa maisha uliotokana na mtikisiko wa uchumi wa nchi hiyo.

Ongezeko kubwa la mfumuko wa bei na gharama ya maisha nchini Ufaransa na kutokuwapo mlingano baina ya gharama za matumizi na mapato ya sehemu kubwa ya Wafaransa, kumesababisha pia wimbi la migomo katika nchi hiyo ya Ulaya.

Wafaransa katika maaandamano mjini Paris

Wafanyakazi nchini Ufaransa wanalalamikia ongezeko la umri wa kustaafu kutoka umri wa miaka 62 ya sasa hadi miaka 65 katika sheria hiyo tatanishi.

Haya yanajiri wakati huu ambapo migomo ya wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi imelemaza usafiri wa umma katika pembe zote za nchi hiyo ya Ulaya, ambayo pia inasakamwa na mgogoro wa nishati, mfumko wa bei na mdororo wa uchumi.

Tags