May 18, 2023 01:17 UTC
  • Upembuzi wa sababu za kuingia katika duru ya pili uchaguzi wa rais wa Uturuki

Kama ilivyokuwa imetabiriwa na duru huru za kisiasa, uchaguzi wa rais wa Uturuki umeingia kwenye duru ya pili na chama tawala cha Uadilifu na Maendeleo (AKP) na muungano wake wa Jamhuri zimeshindwa kupata wingi wa kura zilizohitaji ili kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Tume ya Uchaguzi ya Uturuki imetangaza kuwa: katika uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika kwa pamoja Mei 14, kwa kushiriki asilimia 88.48 ya wapiga kura, kiwango cha juu zaidi cha ushiriki kimerekodiwa katika historia ya uchaguzi wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, ni chini ya asilimia 12 ya Waturuki hawakushiriki katika uchaguzi wa rais. Katika historia ya miaka 100 ya Jamhuri ya Uturuki, ni mara mbili tu imetokea kiwango cha ushiriki kuwa chini ya 70% na kufikia 64%. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Uturuki, kila raia anaweza kupiga kura katika sehemu moja tu iliyoainishwa; na serikali ina haki pia ya kuwatoza faini ya fedha taslimu raia wasiopiga kura. Hata hivyo, sheria hiyo haijawahi kutekelezwa na hakuna mtu yeyote aliyepigwa faini hadi sasa kwa sababu ya kutopiga kura.
Sinan Ogan

Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Uturuki yanaakisi ukweli kwamba, kwa miaka yote hii idadi ya kura za Recep Tayyip Erdoğan imekuwa ikipungua. Kwa mfano, kulingana na matokeo ya uchaguzi uliopita wa rais, Erdoğan aliweza kushinda kiti cha urais wa Uturuki kwa kupata 52% ya kura. Hata hivyo, katika uchaguzi wa urais wa Mei 14 mwaka huu, rais huyo wa Uturuki hakuweza kusherehekea ushindi wake katika duru ya kwanza baada ya kupata chini ya asilimia 50 ya kura. Sababu ya jambo hili iko wazi kabisa. Utekelezaji wa sera zisizo sahihi katika uga wa kiuchumi, hali mbaya iliyojitokeza katika maisha ya watu kwa kuongezeka kwa kasi mfumuko wa bei na kupungua thamani ya sarafu ya taifa, makosa ya mara kwa mara katika sera za nje na utekelezaji wa hujuma za kijeshi kuhusiana na nchi jirani, ni miongoni mwa matatizo yaliyochangia kupungua kura za Recep Tayyip Erdoğan katika uchaguzi wa mwaka huu.

 
Ni dhahiri kwamba katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais – ambao umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi huu wa Mei – rais wa sasa wa Uturuki atakabiliwa na ushindani mkali wa Kemal Kilicdaroglu. Na ni wazi kuwa, katika duru ya pili, iwapo mgombea yeyote kati ya wawili hao ataweza kuwashawishi wananchi ambao hawakushiriki katika duru ya kwanza wajitokeze kumpigia kura katika duru hiyo, basi anaweza tokea sasa kujitambua kama rais ajaye wa Uturuki.
Kutoka kushoto: Erdogan, Kilicdaroglu na Ogan

Lililo wazi ni kwamba mgombea aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais ana nafasi muhimu sana na taathira kubwa katika kuainisha matokeo ya uchaguzi huo. Mgombea huyo Sinan Ogan, ambaye alipata zaidi ya asilimia tano ya kura katika duru ya kwanza, anaweza kumpatia kura zake mgombea yeyote atakayefikia makubaliano naye. Ukweli ni kwamba, Recep Tayyip Erdoğan na Kemal Kılıçdaroğlu wanakabiliwa na hali inayowafanya wahitajie sana msaada wa Sinan Ogan. Kwa maneno mengine ni kuwa, kura za Ogan kwa wagombea hao wawili walioingia katika duru ya pili zina umuhimu mkubwa sana na zinaweza kuamua nani atakuwa rais ajaye wa Uturuki.

 
Mbali na uchaguzi wa rais ambao umeingia kwenye duru ya pili, matokeo ya uchaguzi wa bunge la Uturuki nayo pia yana umuhimu. Kulingana na kura zilizohesabiwa za jumla ya viti 600 vya Bunge la Uturuki, Muungano wa Jamhuri unaoundwa na Chama cha Uadilifu na Maendeleo, Chama cha Vuguvugu la Utaifa na chama cha Refah Mpya cha mtoto wa hayati Najmedin Erbakan, waziri mkuu wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kiislamu, umejipatia jumla ya viti 322 katika Bunge. Pamoja na ukweli kwamba muungano wa Jamhuri umeweza kunyakua viti vingi vya ubunge, lakini ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo ulikuwa na zaidi ya asilimia 53 ya kura zote na viti 342 vya ubunge, muungano huo umepoteza viti 20 katika uchaguzi wa mwaka huu. Muungano wa Taifa unaoongozwa na Kemal Kilicdaroglu unaohesabiwa kama muungano mkuu wa upinzani umeshinda jumla ya viti 212. Wakati huo huo, Muungano wa Leba na Uhuru umenyakua viti 66. Vyama vya Kikurdi, cha Kijani na Mustakbali vya mrengo wa kushoto vimedhoofika kwa kupoteza viti vitano kulinganisha na uchaguzi wa 2018.

Katika tathmini jumla ya uchaguzi wa rais wa Uturuki, inapasa tuseme kuwa: kinachowafanya wananchi wa Uturuki wavutiwe na wagombea ni ahadi zao za kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo. Ni wazi kwamba katika miaka michache ya karibuni, timu ya uchumi ya Erdogan haijaweza kuboresha na kutuliza hali ya mtikisiko iliyoukumba uchumi uliovurugika wa Uturuki. Kwa kweli, Recep Tayyip Erdogan amepoteza fursa zake katika uwanja huo. Na hii ni katika ambayo, shakhsia mashuhuri kama Ali Babajan, ambaye katika muongo wa kwanza wa uongozi wa chama tawala cha Uadilifu na Maendeleo, alichangia sana katika mipango na ustawi wa uchumi wa Uturuki sasa hivi anaongoza timu ya wataalamu wa uchumi ya Kemal Kilicdaroglu.

 
Katika ugawa sera za nje pia, watu kama Ahmet Davutoglu, ambaye huko nyuma alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Erdogan, sasa hivi amejiunga na timu ya Kilicdaroglu. Kutokana na hali hiyo tunaweza kutabiri kuwa katika hali na mazingira ya kawaida, Kılıçdaroğlu ana nafasi nzuri zaidi ya kushinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais na hasa kutokana na kuahidi kwamba atabadilisha sera ya nje ya Uturuki, kwa kuachana na mielekeo ya uanzishaji hujuma na mashambulio ya kijeshi katika ardhi za mataifa mengine.../

Tags