Jun 03, 2023 01:30 UTC
  • Upinzani mkubwa dhidi ya uingiliaji wa London katika masuala ya Waislamu

Idadi kubwa ya Waislamu wamekusanyika mbele ya Kituo cha Kiislamu mjini London wakipinga uingiliaji wa serikali ya Uingereza katika masuala ya Waislamu na kuwekewa mkurugenzi asiye Muislamu kusimamia masuala ya kituo hicho cha ibada.

Washiriki katika maandamano hayo yaliyofanyika mbele ya jengo la Islamic Centre of England wametoa kaulimbiu wakisema: "Acheni Misikiti Yetu", na wamelaani uamuzi wa Tume ya Hisani (Charity Commission) na kueleza wasiwasi wao kuhusu mwenendo wa kuendelea kuingilia masuala ya Waislamu nchini Uingereza.

Tume ya Hisani ya Uingereza, (Charity Commission) chombo ambacho mkuu wake huteuliwa na waziri wa utamaduni na ana jukumu la kusimamia utendaji wa mashirika ya hisani, wiki tatu zilizopita na kufuatia kampeni iliyochochewa na misimamo ya kisiasa dhidi ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza, ilimteuwa wakili wa anayeitwa Emma Moody, ambaye kwa mujibu wa waandamanaji, hana ufahamu sahihi wa maslahi ya umma wa Kiislamu, kuwa usimamizi wa eneo hilo la ibada la Waislamu.Madhumuni ya hatua hiyo ni kuendesha shughuli za Kituo cha Kiislamu cha Uingereza (Islamic Centre of England) kwa mujibu wa maslahi ya serikali ya kihafidhina ya nchi hiyo na kuwasilisha “Uislamu” onaooana na sera za nchi za Magharibi, hususan Marekani.Wakati huo huo, hatua ya Kamisheni ya Hisani ya Uingereza ni ya kisiasa kikamilifu yenye lengo la kuoanisha baina ya sera za London na Washington. Haya yanajiri baada ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza kufanya majlisi ya kusoma khitma na kukumbuka tukio la kuuawa shahidi na kidhulma Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo 2020.

Itakumbukwa kuwa, Disemba mwaka 2022 Charity Commission ilitangaza kuwa imefungua faili la uchunguzi dhidi ya Islamic Centre of England na kutoa tuhuma kadhaa dhidi ya kituo hicho cha Kiislamu.  Awali serikali ya kihafidhina ya Uingereza ilikuwa tayari imetangaza uungaji mkono wake na kuridhia kitendo cha kigaidi cha utawala wa Donald Trump mnamo Januari 3, 2020. Wakati huo, wanajeshi wa Marekani, chini ya amri ya moja kwa moja ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump, waliwaua kigaidi watu wote waliokuwa ndani ya magari mawili yaliyokuwa karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq, kwa kutumia ndege isiyo na rubani. Hujuma hiyo ya kigaidi iliulenga msafara wa Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC, na Abu Mahdi Al-Muhandis, aliyekuwa naibu wa vikosi vya wapiganaji wa kujitolewa vya al Hashdu al Shaabi vya Iraqi.

Waislamu UK wanavyokandamizwa na vyombo vya usalama hadi ndani ya Misikiti

Katika taarifa iliyochapishwa Mei 10, 2023, mkuu wa Tume na Hisani ya Uingereza alidai kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda nafasi ya "hisani" katika fikra za umma, na kwamba mkurugenzi huyo wa muda atafanya jitihada za kuboresha kazi ya usimamizi wa kituo hicho.Kwa njia hii, Charity Commission ya Uingereza, inadhani kwamba imefanya juhudi za kukiondoa Kituo cha Kiislamu cha Uingereza mikononi mwa wale waliokuwa wakifanya kazi ya kuendeleza Uislamu halisi wa Mtume Muhammad (SAW).Waandamanaji waliokusanyika mbele ya Kituo cha Kiislamu cha Uingereza Alkhamisi usiku walisisitiza kuwa taasisi za serikali hazina haki ya kuainisha wajibu wa kiitikadi wa jamii za kidini na kwamba hatua ya Tume ya Hisani ya Uingereza pia inatambuliwa kuwa ni uingiliaji usio na mantiki katika masuala ya Kiislamu.

Kwa msingi huu, waandamanaji wametoa wito wa kufutwa uamuzi wa Tume ya Hisani wa kumteua mtu asiye Mwislamu kusimamia kazi za kituo hicho cha ibada za Waislamu, na kuacha kuingilia masuala ya vituo vya Kiislamu.

Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza anasema: Tume ya Hisani ya Uingereza imeweka mashinikizo kwa misikiti na vituo vya Kiislamu vya nchi hii ili kuzima shughuli zao za kidini na kusitisha utekelezaji wa majukumu ya vituo hivyo. "Wanataka kuudhibiti Uislamu halisi wa Mtume wetu Muhammad (SAW) na badala yake waweke Uislamu bandia unaoendana na kanuni za Magharibi", amesisitiza Shajareh.Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza anasema kosa la maafisa wa Kituo cha Kiislamu cha Uingereza ni kutosalimu amri na kukataa kutekeleza maagizo na amri zisizo halali za Charity Commission na ameeleza wasiwasi wake kuhusu mustakbali wa Uislamu katika nchi za Magharibi. Amesisitiza kuwa: “Iwapo hatutasimama na kutetea  imani na itikadi zetu, watadhoofisha Uislamu wetu na kuweka nakala ya ‘Uislamu wa Kiingereza’ mahali pake.

Nukta muhimu ni kwamba, hatua inayokiuka sheria na ya kichochezi ya Tume ya Hisani ya Uingereza dhidi ya Islamic Centre of England pia imekabiliwa na upinzani wa waumini wa dini nyingine za Kiibrahimu. Kuhusiana na hili, Jumatano iliyopita wawakilishi wa makumi ya taasisi za Kiislamu, wanataaluma na wanaharakati wa Kikristo na Kiyahudi walisema katika barua ya pamoja iliyotumwa kwa Mkuu wa Tume ya Hisani ya Uingereza kwamba sio jukumu la chombo chochote cha serikali kuziambia jumuiya za kidini nini cha kusema na kuamini katika maeneo yao ya ibada. Waandishi wa barua hiyo walieleza kuwa matokeo ya vitendo kama hivyo ni kuzidisha chuki dhidi ya Uislamu na kuwalazimisha Waislamu kukaa mbali na maeneo yao ya ibada.

Tags