Jun 09, 2023 01:24 UTC
  • Rais wa Kazakhstan ataka kufanyiwa mageuzi Baraza la Usalama

Rais wa Kazakhstan ametoa mwito wa kufanyiwa mageuzi muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan alitoa mwito huo jana Alkhamisi katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Astana na kuongeza kuwa, "UN inasalia kuwa shirika kubwa zaidi linaloziunganisha nchi zote duniani, lakini taasisi hiyo haiwezi kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali pasi na kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama."

Rais Tokayev amenukuliwa na shirika la habari la Russia Today akisema kuwa, mzizi wa ukosefu wa uthabiti unaoshuhudiwa hivi sasa duniani ni wa jadi, na kwamba mifarakano iliyopo duniani hivi sasa si tu ya kijiopolitiki, bali pia ya kiuchumi. 

Kuweko mabadiliko katika mfumo wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kilio cha muda mrefu hasa kutoka kwa mataifa yanayostawi kama vile ya Afrika.

Baraza la Usalama la UN

Kadhalika Rais wa Kazakhstan amelalamikia dhulma katika muundo wa Baraza la Usalama la UN na kukisisitiza kwamba, si haki kwa nchi tano tu hasa za Magharibi kuwa na haki ya kura ya veto.

Wakati mabara ya Amerika, Ulaya na Asia yana nchi ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bara la Afrika ndilo pekee ambalo halina uwakilishi wa uanachama wa kudumu kwenye chombo hicho chenye sauti ya juu ndani ya umoja huo.

Tags