China: Tutaendelea kuunga mkono kadhia ya Palestina
-
Wang Wenbin
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China amesema Beijing itaendelea kuunga mkono mapambano halali ya Wapalestina ya kupigania haki zao za kitaifa, na kusisitiza kwamba kadhia ya Palestina ni katika masuala muhimu ya eneo la Asia Magharibi.
Wang Wenbin amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, China na Palestina zina uhusiano wa kidugu wa jadi. Amesema China ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kuitambua Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na dola la Palestina.
Kuhusu safari tarajiwa ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina nchini China, Wenbin amesema: Mahmoud Abbas ni rafiki mzuri na mkongwe wa taifa la China, na atakuwa mmoja wa viongozi wa Kiarabu kupokewa na China mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China ameongeza kuwa, hatua ya China kuwa mwenyeji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inaashiria urafiki wa karibu baina ya Wachina na Wapalestina.

Kadhalika ameutaka utawala haramu wa Israel ukomeshe mara moja tabia yake ya uchokozi, kuchochea taharuki na kupora ardhi na rasilimali za Wapalestina hasa katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Amesema taharuki imeshtadi eneo la Mashariki ya Kati tangu utawala wa Kizayuni uchukue hatua ya kusaini agizo la kubariki ujenzi zaidi ya vitongonji vya walowezi wa Kiyahudi kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
Rais Xi Jinping wa China hivi karibuni alisisitiza kwamba ukandamizaji wa kihistoria wanaofanyiwa watu wa Palestina haupaswi kuendelea kwa muda usiojulikana na kwamba haki halali na za kitaifa za Wapalestina hazipaswi kuathiriwa.