Jul 03, 2023 08:14 UTC
  • Ubaguzi wa rangi; Mgogoro mkubwa barani Ulaya

Kuendelea na kushadidi sera za ubaguzi umekuwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kijamii barani Ulaya, kiasi kwamba katika miezi ya hivi karibuni raia wengi wa Ulaya wametoa wito wa kukomeshwa sera hizo kwa kufanya mikutano na maandamano.

Kuongezeka migogoro ya kijamii kumepelekea viongozi wa Ulaya kukiri kivitendo kuwepo kwa sera hizo za ubaguzi wa rangi akiwemo Kansela wa Ujerumani Olaf Schultz ambaye amekiri ukweli huo kwa kusema: Kwa bahati mbaya, ubaguzi wa rangi ni hakika nchini Ujerumani, hivyo Wajerumani wanapaswa kutafuta njia za kukabiliana na tatizo hili kwa pamoja.

Ubaguzi wa rangi umekuwa tatizo kubwa barani Ulaya. Kuenea ubaguzi huo katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, kumesababisha hali ya kutoridhika kijamii kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni. Tatizo hilo sambamba na kushadidi matatizo ya kiuchumi na kisiasa katika nchi hizo yameibua mzozo mkubwa katika baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Ufaransa.

Kulingana na sheria za nchi nyingi za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, hakuna mtu anayepaswa kunyimwa haki za kijamii, kisiasa au kiuchumi kwa sababu ya rangi ya ngozi, dini, umri wala ulemavu. Lakini ukweli wa sasa wa nchi za Ulaya unaonyesha kuwa sheria hizi mara nyingi hubaki kwenye karatasi tu. Kwa kweli, nchi za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, hukiuka sharia zilizopo za usawa. Mashirika yasiyo ya kierikali yanayopambana na ubaguzi wa rangi yanasema kwamba raia wa Ufaransa wenye asili ya Kiafrika na Kiarabu ndio wahanga wakuu wa ubaguzi wa rangi katika nchi hiyo. Kitendo cha afisa wa polisi wa Ufaransa kumuua Nael Marzouq, kijana mwenye asili ya Algeria katika siku za hivi karibuni, kwa mara nyingine tena kimeigeuza Ufaransa kuwa uwanja wa machafuko na maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi.

Hivi sasa raia wengi wa Ufaransa wamejitokeza mitaani kupinga sera hizo, na katika siku chache zilizopita, miji mingi ya nchi hiyo imekuwa uwanja wa maandamano na makabiliano ya polisi na waandamanaji. Maandamano hayo kimsingi yameipoozesha Ufaransa na kuzifanya nchi nyingine za Ulaya kuingiwa na hofu kubwa, kwa namna ambayo Nancy Faeser, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, amekiri kwamba Waislamu wengi wa nchi hiyo wanakabiliwa na ubaguzi na suala hili linaongeza chuki katika jamii.

Cihan Sinanoglu, mtafiti wa sayansi ya jamii katika uwanja huo, anasema: "Takwimu husema ukweli." Ubaguzi wa rangi nchini Ujerumani si jambo la pembeni, bali ni jambo linaloathiri jamii nzima.

Ripoti zilizochapishwa zinaonyesha kwamba wahamiaji wengi weusi au wenye asili ya Afrika katika nchi za Ulaya wanadhibitiwa vikali na polisi, na wengi wanapigwa na polisi bila kuthibitisha uhalifu. Pia, watu weusi katika baadhi ya nchi za Ulaya wako katika makundi ya chini ya kazi na wengi wao hawapati haki wanazostahiki kulingana na nafasi zao za kazi. Katika muktadha huu, hata watu mashuhuri kama Vinicius, nyota mweusi wa Brazil mwenye umri wa miaka 22 wa timu ya Real Madrid, hawajaepushwa na tabia hizi za kibaguzi.

Kwa upande mwingine, kuenea chuki dhidi ya Uislamu kumewafanya Waislamu katika nchi za Ulaya wakabiliwe sio tu na ubaguzi bali pia na ukosefu wa usalama. Utafiti wa "Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kiislamu" unaonyesha kuwa asilimia themanini ya Waislamu nchini Uingereza wanaamini kuwa wao ni wahanga wa chuki dhidi ya Uislamu. Takwimu rasmi za Kituo cha Kitaifa cha Wafanyakazi cha Uingereza pia zinaonyesha kuwa Waislamu 7 kati ya 10 wanaofanya kazi nchini Uingereza walisema walikabiliwa na aina fulani ya vitendo vinavyoashiria chuki dhidi ya Uislamu.

Sasa, ukosefu wa usawa, ubaguzi, na matatizo mengi ya kijamii yamekuwa sababu ya maandamano makubwa katika nchi kadhaa za Ulaya, ambayo nyakati fulani hugeuka kuwa ghasia zenye uharibifu na machafuko kama yale yanayoshuhudiwa hivi sasa nchini Ufaransa.

Tags