Apr 09, 2019 12:13 UTC
  • Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia Iran

Tarehe 20 Farvardin Inasadifiana na "Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia" nchini Iran. Katika siku kama hii mwaka 1385 Hijria Shamsia sawa na Aprili 9 2006, wanasayansi na wasomi Wairani walifanikiwa kukamilisha mzunguko wa utegenezaji fueli ya nyuklia katika maabara.

Baada ya kutangazwa habari ya mafanikio hayo ya wasomi na wanasayansi Wairani katika urutubishaji urani na kuzinduliwa mchakato kamili wa urutubishaji urani kwa kutumia mashinepewa au centrifuge zilizoundwa nchini Iran, Shirika la Kimataifa la Nishati Atomiki IAEA liliitangaza Iran  kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimeweza kumiliki teknolojia ya kurutubisha urani katika uga wa shughuli za nyuklia kwa malengo ya amani.

Kufuatia mafanikio hayo makubwa ya kisayansi, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni nchini Iran lilipasisha azimio kuwa, katika kuenzi na kushukuru jitihada zilizojaa fahari za wasomi Wairani katika kuiwezesha nchi hii iweze kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani, tarehe 20 Farvardin itakuwa 'Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia.'

Teknolojia ya nyuklia sasa inahesabiwa kuwa miongoni mwa sayansi za ngazi za juu zaidi. Leo taathira chanya ya elimu ya nyuklia katika maisha ya mwanadamu ni jambo lisiloweza kupingika na ni msingi muhimu na wa dharaura katika maendeleo endelevu.

Rais Hassan Rouhani akizundua mafanikio ya nyuklia katika sherehe za Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia mwaka 2017

 

ujipatia teknolojia ya nyuklia kwa kuzingatia Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia maarufu kama NPT ni haki ya kisheria ya kila nchi ambayo inafungamana na mkataba huo. Hivi sasa duniani, kuna nchi takribani 10 ambazo zimeweza kumiliki ujuzi kamili wa kisayansi wa teknolojia ya nyuklia. Nishati ya nyuklia ina matumizi mengi sana na ni kwa msingi huo ndio hadi sasa kumiliki elimu ya nyuklia ni tamanio na lengo la nchi nyingi sana.

Katika kipindi cha nusu karne iliyopita, teknolojia ya nyuklia imekuwa na nafasi muhimu sana katika ustawi wa viwanda, kilimo na tiba.

Kati ya matumizi muhimu ya elimu ya nyuklia ambayo tunaweza kuyataja hapa ni katika uundwaji wa radioisotope ambazo ni muhimu katika kutambua na kutibu magonjwa sugu, kuzalisha umeme na pia katika kuimarisha mazao ya kilimo n.k.

Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran anasema: "Katika kipindi cha miaka 10 tulitaka kununua urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20  na tuliandika barua rasmi kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na tukawekewa masharti mengi. Katika kipindi hicho nilifika kwa Bw. El Baradei ambaye wakati huo alikuwa Mkurungezi Mkuu wa IAEA na tukafanya mazungumzo. El Baradei alinionyesha barua isiyo rasmi ambayo ilikuwa imeandikwa na Marekani pamoja na Russia. Katika barua hiyo walikuwa walituwekea masharti mengi sana ambayo tulipaswa kuyatekeleza na hivyo hawakutupatia urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20. Baada ya hapo tukaamua kuchukua hatua za kujirutubishia wenyewe urani kwa kiwango cha asilimia 20. Kama hatungefanya hivyo tanuri nyuklia yetu ya Tehran ingesitisha kazi zake na tungekumbana na matatizo katika utengenezaji wa radioisotope. "

Katika zama hizo walikuwa wakisema Iran haina uwezo wa kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20. Lakini walishangaa wakati walipoona kuwa katika kipindi cha chini ya miaka miwili Iran ilipata mafanikio makubwa na hivi sasa Tanuri Nyuklia ya Tehran inatumia urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi. Katika muendelezo wa mafanikio hayo, mapema mwezi Januari mwaka huu wa 2019, kwa mara ya kwanza kabisa Iran ilifanikiwa kuzalisha fueli ya kisasa ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa ajili ya Tanuri Nyuklia ya Tehran.

Mafanikio hayo makubwa yamepatikana katika hali ambayo Marekani imekuwa ikifanya juu chini kuhakikisha kuwa inaipa Iran pigo ili kusimamisha mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

Katika mchakato wake wa "Elimu ya Nyuklia", Iran imelipa gharama kubwa na kupata hasara za kisiasa, kisheria na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuuawa shahidi wanasayansi wake wanne wa nyuklia ambao ni Mustafa Ahmadi Roshan, Masoud Ali Mohammadi, Majid Shahriyar, na Dariush Rezainejad. Wanasayansi hao Wairani waliuaawa shahidi katika oparesheni za maajenti  ajinabi.

Halikadhalika kumekuwa kukitekelezwa njama kadhaa za uvurugaji katika mpango wa nyuklia wa Iran. Mfano wa hilo ni kutumiwa kirusi hatari cha Stuxnet ambacho kilijipenyeza katika kompyuta zinazohusika na shughuli za nyuklia za Iran. Lakini pamoja na njama hizo zote, taifa la Iran kamwe halitalegeza msimamo katika haki yake isiyopingika ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Rais Donald Trump wa Marekani  Mnamo Mei 8 2018, hatimaye, baada ya vitisho vya muda mrefu aliiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA. Baada ya hatua hiyo alitangaza kuanza tena kutekelezwa vikwazo dhidi ya Iran ambavyo vilikuwa vimesimamishwa kufuatia mapatano hayo.

Baada ya kufikiwa mapatano ya JCPOA mwaka 2015, Iran ilijitolea na kukubali kujiwekea vizingiti vya nyuklia na ikawa inashirikiana kikamlifu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Lakini pamoja na hatua hizo chanya, Marekani imeendelea kutekeleza njama za kuizuia Iran inufaike na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Ni kwa sababu hii ndio, mapatano ya JCPOA bado hayajaweza kukidhi maslahi halali ya Iran katika uga wa nyuklia na pia hajaweza kupelekea nchi hii iondolewe vikwazo. 

Nchi za Umoja wa Ulaya, China na Russia ambazo pia zimo katika mapatano ya JCPOA, ziliikosoa vikali Marekani kwa kujioondoa katika mapatano hayo na pia wakati huo huo zikaiomba Iran isichukue uamuzi sawa na huo wa Marekani. Pande zote ziliafiki kuhakikisha kuwa mapatano ya JCPOA yanaendelea bila ya Marekani kuwepo. Iran ilikubali ombi hilo kwa sharti kuwa maslahi yake katika JCPOA yalindwe.

Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran katika mahojiano na Euronews alisema:

"Iwapo Iran itaamua kujiondoa JCPOA na kurejea katika hali ya kabla ya mapatano katika uga wa nyuklia, mbali na kurutubisha urani kwa asilimia 20 katika muda wa siku mbili, tunaweza pia kuzindua kiwanda cha kuzalisha chuma ya urani.

Mashinepewa (centrifuge) zilizoundwa nchini Iran

Iran na nchi tatu za Umoja wa Ulaya, yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa, zimeanzisha  Mfumo Maalumu kwa ajili ya Mabadilishano ya Kifedha baina ya Iran na Ulaya, kwa Kiingereza Special Purpose Vehicle,(SPV). Kwa mujibu wa mfumo huu taasisi za kifedha, benki na mashirika madogo ya kibiashara ya Ulaya yanaweza kufanya kazi na Iran pasina kulengwa na vikwazo vya Marekani. Inatazamiwa kuwa mapatano hayo yataimarisha biashara ya Iran katika uga wa kimataifa. Lakini hadi sasa mfumo huu haujaweza kutenda kazi kama ilivyotarajiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei,  wakati akihutubia umati mkubwa wa watu katika Haram ya Imam Ridha AS katika mji mtakatifu wa Mashhad ulioko kaskazini mashariki mwa nchi katika siku ya kwanza ya Nowruz (Machi 21) aliashiria jinsi nchi za Ulaya zilivyoshindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu kuanzisha kanali maalumu ya mabadilishano ya kifedha baina ya Iran na Ulaya.  Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: "Uzoefu wa kihistoria na ushahidi wa wazi wa vitendo vya Wamagharibi unaonesha kuwa mtu anaweza kutarajia kutoka kwao njama, usaliti na kushambulia kwa nyuma lakini hawezi kutegemea kutoka kwao urafiki na ushirikiano wa kweli."

Leo jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika orodha ya nchi chache duniani zenye kumiliki elimu na ujuzi wa nyuklia. Tarehe 20 Farvardin ni Siku ya Kitaifa ya Nyuklia  nchini Iran. Siku hii inakumbusha kuhusu irada imara ya taifa kubwa la Iran ambalo limesimama kidete mbele ya madola makubwa yatumiayo mabavu katika kutetea haki yake isiyopingika ya kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo  ya amani.

 

Tags