Sep 30, 2023 02:26 UTC
  • Jumamosi, 30 Septemba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 30 Septemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 8 Mehr, ni maarufu hapa nchini Iran kama siku ya kumuenzi Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi. Maulana Jalaluddin alizaliwa mwaka 604 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh uliokuwa moja kati ya miji ya Iran ya kipindi hicho. Moulavi alikuwa gijwi wa mashairi na malenga mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Maanavi. ***

Maulana

 

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia. Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya kila aina ya jinai na alitambulikana kwa ufuska. Miongoni mwa jinai zake ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali (AS) na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina na kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba. ***

 

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hussein Tabatabai Qomi, fakihi na marjaa mahiri wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1282 Hijria katika mji mtakatifu wa Qom ulioko yapata kilomita 125 kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran. Alisoma masomo yake ya utangulizi na ya msingi ya dini katika mji huo. Baadaye Sayyid Tabatabai alielekea Tehran na kunufaika na drsa na masomo ya Maulamaa wa mji huo. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alifunga safari na kwenda katika Hawza ya Najaf nchini Iraq. Mwanazuoni huyu hakuwa nyuma pia katika uandindishi wa vitabu na baadhi ya vitabu vyakke ni Manasik Haj, Dhakhirat al-Ibad na Tariq al-Najat. ***

Sayyid Hussein Tabatabai Qomi

 

Miaka 57 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia. ***

Bendera ya Botswana

 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika. ***

Charles Richter

 

Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina hilo ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo. ***

Siku ya Kimataifa ya Viziwi.

 

Tags