Dec 05, 2023 02:39 UTC
  • Jumanne, tarehe 5 Disemba, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 21 Jumadil Awwal 1445 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2023.

Miaka 1124 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qirawani, aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Ibn Jazzar. Msomi huyo wa Morocco alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu kheri na aliandika kitabu alichokipa jina la "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.

Ibn Jazzar

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, aliaga dunia Alexandre Dumas mwandishi mtajika wa Kifaransa. Mwandishi huyo ambaye ni mashuhuri pia kwa jina la Dumas Baba baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa katika ofisi moja ya kiwanda kama katibu kutokana na kuwa na hati nzuri.

Alexandre Dumas

Katika siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar. Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.   

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo,  alizaliwa Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni mwa kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears. 

Walt Disney

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Nelson Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Baada ya kushika hatamu za uongozi, Mandela aliamiliana vyema na watala wa zamani wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na hata wale waliomfunga jela na kumtesa. Mwenendo huo wa kusamehe ulizidisha umashuhuri na kupendwa shujaa huyo, na mwaka 1993 alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel. Kitabu mashuhuri zaidi cha shujaa huyo wa Afrika ni kile chenye kumbukumbu zake alichokipa jina la: "Njia Ndefu ya Kuelekea kwenye Uhuru".   

Nelson Mandela

Na leo, Disemba 5, ni Siku ya Kimataifa ya Wahisani ambao hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine. Kutenda wema na kufanya hisani ni suala ambalo halihusu, dini, taifa, wala kaumu makhsusi. Hata hivyo Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, umehimiza zaidi kutenda wema na hisani na kuwataja wahisani na watenda wema kwamba ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 195 ya Suratul Baqara inasema: Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wahisani.   

 

Tags