Jul 10, 2016 06:27 UTC

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine umewadia wa kuwa nanyi wapenzi wasikilizaji katika dakika chache za kipindi hiki cha kila wiki. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia maudhui ya kifo na mauti na maisha ya milele ya wanadamu. Tulisema kuwa, kupitia kifo na mauti, mwanadamu huhamia katika ulimwengu mwingine wa Akhera katika safari yake ya kufikia ukamilifu.

Kwa msingi huo kuna ulazima wa wanadamu kujitayarisha kwa ajili ya maisha ya milele katika ulimwengu wa Akhera. Kukumbuka kifo na mauti kuna nafasi kubwa sana katika uwanja huo. Mtume SWA anasema: Muumini hodari zaidi kuliko wote ni yule anayekumbuka mauti zaidi na kujitayarisha kwa ajili ya kifo. (Biharul Anwar: juzuu 2)

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha leo kitazungumzia umuhimu wa kukumbuka mauti na kifo daima na taathira zake katika maisha ya mwanadamu. Karibuni….

Maisha na hamu ya mwanadamu na kubakia hai hapa duniani ni miongoni mwa hakika ambazo haziwezi kupuuzwa na kufumbiwa macho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uhai ni jambo zuri na linalopendwa na wanadamu wote na kila kiumbe hufanya jitihada kubwa kwa ajili ya kubakia hai na kuishi. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Eleweni kwamba, hakuna kitu ambacho mwanadamu hakishibi na kukikinai isipokuwa uhai kwa sababu kidhahiri mwanadamu hajihisi raha katika mauti….”. (Nahjul Balagha:133) Hii ina maana kwamba, mwanadamu yeyote na katika vipindi na nyakati zote za furaha na ghamu, uzima na ugonjwa na kadhalika hupenda uhai na kubakia hai. Hata hivyo inatupasa kuelewa kwamba, kubakia hai hapa duniani si lengo la maisha ya mwanadamu bali ni wenzo na njia ya kuelekea kwenye uhai na maisha ya milele katika ulimwengu mwingine. Pamoja na hayo watu wengi hushughulishwa na maisha haya ya dunia na kuyafanya lengo lao la mwisho na asili. Mhenga mmoja anasema: Maisha ya dunia ni mithili ya maji ya chumvi ambayo kadiri mwanadamu anavyoyanywa ndivyo kadiri anavyopata kiu zaidi. Mwanadamu katika kutafuta dunia ni kama nondo wa hariri (silkworm) kadiri anavyozalisha tando za hariri, hujifunga tando hizo na mwishowe huwa vigumu kwake kujinasua katika uzi hizo za hariri”.

Lengo la kukumbuka mauti daima si kuacha kutumia ladha za dunia bali ni kumfanya mwanadamu apange na kuratibu maisha yake hapa duniani kwa njia itakayomfikisha kwenye saada na ufanisi wa Akhera na aweze kufaidika na ladha za dunia hii na ulimwengu mwingine wa juu zaidi. Maisha ya dunia ni neema kubwa kwa mwanadamu, na Akhera yake inaundika kutokana na matendo na mwenendo wake hapa duniani. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) anasema: “Dunia ni shamba la Akhera…”. Kwa msingi huo kuna udharura kwa mwanadamu kuwa na uadilifu na mwenendo wa kati na kati katika maisha yake. Wasii wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Twalib anasema: Mtu anayetosheka kwa machache ya dunia hujitengenezea mengi ya kumlinda, na anayetumia na kujilimbikizia mengi ya dunia huwa amejitengenezea mengi ya kumuangamiza. (Nahjul Balagha:111)

Kwa msingi huo Mwislamu wa kweli ni yule ambaye sambamba na kuupa mazingatio na umuhimu uhai na maisha haya ya kupita, hupanga ratiba na utaratibu wa kumfikisha katika maisha na uhai wa milele. Viongozi wetu wa dini hususan Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu hawakuacha hata dakika moja katika maisha yao bila ya kujishughulisha na kazi muhimu. Kwa mfano tu baada ya Mtume kufariki dunia, Imam Ali bin Abi Twalib (as) alijishughulisha na kazi ya kilimo na kuchimba visima. Anasimulia kuhusu kazi zake katika kipindi hicho cha kabla ya kushika hatamu za uongozi kwamba: “Wakati mmoja nilikuwa nikifunga jiwe tumboni mwangu kutokana na njaa na sasa kila mwaka ninatoa sadaka dinari elfu arubaini”. Hii ina maana kwamba, Imam Ali (as) daima alikuwa akifanya kazi za uzalishaji lakini kamwe hakutekwa na kusalitika na maisha ya kupita ya dunia na vishawishi vyake. Imam Ali (as) daima alikuwa akisisitiza udharura wa kuwa na uadilifu na njia ya kati na kati maishani. Anasema katika barua aliyomwandikia Muhammad bin Abu Bakr wakati alipomteua kuwa gavana wake nchini Misri kwamba: Wachamungu wameishi katika maskani nzuri zaidi za dunia na kula mazuri yake zaidi. Wamefaidika na neema za dunia sawa na walioneemeshwa na kuchukua humo waliyochukua majabari wenye kiburi lakini waliihama dunia wakiwa na masurufu ya kutosha na biashara yenye faida. Wamepata ladha ya uchamungu katika dunia yao na wakapata yakini kwamba, watakuwa pamoja na Mwenyezi Mungu kesho katika Akhera yao…. Kuweni na hadhari na mauti enyi waja wa Mwenyezi Mungu na jitayarisheni kwa ajili yake… Hakika mnakimbizwa na mauti. Mkisimama yanawakumba, na mukikimbia yanakuta.. Tahadharini na moto wenye kina baidi, joto shadidi na adhabu jadidi”. (Nahjul Balagha:Barua ya 27)     <<<< >>>>>

Katika Qur’ani tukufu, hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu kumesisitizwa sana suala la kuwa macho mwanadamu na kutotekwa na maisha ya kupita ya dunia na ladha na anasa zake na dharura wa kupenda na kuashiki maisha ya kudumu na ya milele huko Akhera. Msisitizo huo mkubwa uliokaririwa sana katika mafundisho ya Uislamu unafanyika ili mwanadamu asisahau kuwa, maisha ya dunia hii ni mafupi sana licha ya ladha zake. Hivyo mwanadamu anapaswa kutumia vyema na katika njia sahihi umri wake hapa duniani.

Hata hivyo kuna mambo mengi yanayomfanya mwanadamu asahau na kughafilika na uhakika huo na umuhimu wa maisha ya kudumu katika ulimwengu wa Akhera. Miongoni mwa mambo yanayomghafilisha mwanadamu na kumsahaulisha mauti na kifo ni kuwa na maratajio makubwa ya maisha ya dunia na kubakia kwake. Matarajio ya kubakia muda mwingi na kuwa na umri mrefu hapa duniani ni miongoni mwa maadui wakubwa zaidi wa saada na maisha bora na ya kudumu huko Akhera. Hii ni kwa sababu tajiriba na uzoefu wa historia umeonesha kuwa, mwanadamu hana mpaka katika matarajio yake na kadiri siku zinavyopita ndivyo anavyozama zaidi katika matarajio na matamanio yake. Ni wazi kuwa matarajio hayo ya kuwa atabakia na kuishi maisha marefu huchukua sehemu kubwa ya nguvu na uwezo wake wa kifikra na kimwili na kumzamisha zaidi katika dunia na ladha zake, na wakati huo huo kumsahaulisha Akhera na maisha ya baadaye na ya milele. Matarajio hayo humfanya atekwe na dunia na kumsahaulisha suala la kujiandaa kwa ajili ya mauti na Akhera. Imam Ali (as) anasema: Enyi watu! Ninachelea zaidi mambo mawili juu yenu: Kufuata matamanio ya nafsi na kuwa na matarajio ya kuishi muda mrefu. Kufuata matamanio ya nafsi humuondoa mwanadamu katika njia ya haki, na matarajio ya kuishi muda mrefu humsahaulisha Akhera”. (Nahjul Balagha: hotuba-42)

Hata hivyo tunapaswa kuweka wazi hapa kuwa, asili ya mtu kuwa na matarajio si jambo baya bali lina nafasi na mchango muhimu katika harakati ya maisha na maendeleo ya kimaada na kiroho ya wanadamu. Mtume Muhammad (saw) amesema: Matarajio ni rehma kwa Umma wangu na kama si matarajio basi hakuna mama ambaye angemnyonyesha mtoto wake, wala hakuna mkulima ambaye angepanda mche ardhini”. (Biharul Anwar: juzuu 74)

Huwenda pia miongoni mwa sababu za kufichwa siku ya mwisho ya umri wa mwanadamu ni kubakisha taa ya matarajio katika nafsi ya kiumbe huyo na kumfanya adumishe juhudi na bidi katika maisha yake.

Imepokewa kutoka kwa Nabii Issa Masiih (as) kwamba alikuwa ameketi sehemu moja ambako alimuona mzee akilima ardhi kwa sepetu na kujishughulisha na kilimo. Mtukufu Issa (as) alimuomba Mwenyezi Mungu akisema: Mola wangu Mlezi! Mnyang’anye matarajio bwana huyu. Ghafla mzee yule alirusha chini sepetu na kulala juu ya ardhi. Muda mfupi baadaye Nabi Issa (as) alimuomba tena Mwenyezi Mungu akisema: Mola wangu! Mrejeshee matarajio mzee huyu. Ghafla alimuona mzee akiinuka na kuanza tena kazi ya kilimo shambani kwake! Nabii Issa alimkaribia na kumuuliza sababu ya suala hilo. Mzee alisema: Awali nilifikiria kwamba, mimi ni mzee asiye na nguvu na uwezo, ninapigwa na jua na ninaweza kufariki dunia leo au kesho. Hivyo basi kwa nini ninajihangaisha na kufanya kazi hizi zote?! Wakati huo nilitupa sepetu chini na kulala.

Baadaye kidogo nilifikiria tena na kujiuliza, hivi kweli haiwezekani mimi nikaishi umri mrefu zaidi? Mbona kulikuwapo watu kama mimi ambao waliishi umri mrefu? Mwanadamu hai anataka kuishi maisha ya heshima na analazimika kufanya bidii kwa ajili yake mwenyewe na familia yake. Wakati huo niliinuka na kushika sepetu na kuanza tena kilimo”. (Biharul Anwar, juzuu 14)

Kwa hakika ni matarajio haya ndiyo yanayompa mwanadamu harakati na utanashati wa kufanya kazi na mambo mengine ya maendeleo lakini matarajio hayo yanapochupa mipaka huwa mithili ya mafuriko yenye uharibifu yanayomgharikisha mwanadamu katika kuabudu dunia, matamanio ya nafsi na dhulma. Kwa msingi huo kukumbuka kifo na mauti kunaweza kupunguza na kudhibiti matarajio ya mwanadamu na kumfanya ajitayarishe kwa ajili ya maisha ya kudumu ya Akhera.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa hadithi kutoka kwa Mtume Muhammad (saw). Siku moja Mtume (saw) alichukua vijiti vitatu na kuchomeka kimojawapo mbele yake ardhini. Alichukua cha pili akakizamisha ardhini kando ya kile cha kwanza na cha tatu akakichomeka ardhini mbali na vijiti hivyo viwili. Kisha aliwauliza maswahaba zake kwamba, munajua hiki ni kitu gani? Walisema: Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua zaidi. Alisema: kijiti cha kwanza ni mwanadamu, cha pili ni mwisho wa umri wake na cha tatu kilichoko mbali ardhini ni matarajio marefu ya mwanadamu anayoyatafuta na kuyafuatilia lakini mauti yanamfika na hafanikiwi kupata matarajio yake.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.  

 

Tags