Aug 06, 2016 04:45 UTC
  • Jumamosi, Agosti 6, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe Tatu Mfunguo Pili Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 6 Agosti mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo 71 iliyopita Marekani, kwa mara ya kwanza iliushambulia kwa mabomu ya nyuklia na kuusambaratisha mji wa Hiroshima huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya uharibifu ya mada za TNT zenye uzito wa tani elfu 20. Katika mashambulizi hayo watu zaidi ya elfu tisini waliuawa na wengine 75 elfu kujeruhiwa. Licha ya kupita miaka 71 sasa tangu Marekani ifanye mashambulizi hayo ya silaha za nyuklia katika mji wa Hiroshima huko Japan, lakini athari zake mbaya bado zinaendelea kushuhudiwa hadi hii leo. Muda mfupi baada ya kuushambulia mji wa Hiroshima, Marekani iliushambulia pia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Nagasaki huko huko Japan. Maafa hayo ya kutisha yaliyofanywa na Marekani katika miji miwili ya Japan yanaonyesha hatari ya kumilikiwa silaha za nyuklia na nchi zinazopenda kujitanua duniani kama Marekani na ndiyo maana kuna udharura wa kusimamiwa na kudhibitiwa silaha hizo na taasisi husika na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa ajili ya usalama wa dunia. ***

Katika siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alizaliwa Alexander Fleming tabibu, mwanabiolojia na mtaalamu wa dawa wa Scottland. Tabibu huyo pamoja na wasomi wenzake wawili Chain na Florey waligundua mada ya dawa ya antibiotic yaani Penicillin wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mwaka 1945, wasomi hao watatu kwa pamoja walitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya tiba kutokana na ugunduzi wao huo muhimu. Penicillin inatumika sana katika elimu ya tiba. ***

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, Jamaica inayopatikana huko Amerika ya Kati ilipata uhuru. Jamaica iligunduliwa mwaka 1494 na mvumbuzi Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania kuanzia karne ya 16 hadi ya 18. Nchi hiyo baadaye ilikoloniwa na Uingereza; na wavamizi wa Ulaya wakawafukuza wenyeji wa kisiwa hicho na badala yake wakawachukua makumi ya maelfu ya watumwa weusi kwa ajili ya kuwalimia mashamba yao. ****

Na katika siku kama ya leo miaka 817 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa Ibn Munir, fakihi na mfasiri wa Kiislamu wa nchini Misri. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Alexandria. Alisoma masomo ya awali na utangulizi kwa baba yake na kasha baadaye akaanza kuhudhuria masomo mbalimbali kama fikihi, fasihi ya lugha na Uluum al-Qur'ani kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Ibn Munir alikipitisha kipindi cha maisha yake akishikilia nyadhifa mbalimbali ambapo kipindi gfulani alikuwa kadhi. Ibn Munir aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 63 huko Alexadria.

 

 

 

Tags