Aug 27, 2025 02:26 UTC
  • Jumatano, tarehe 27 Agosti, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 3 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Agosti 27 mwaka 2025.

Siku kama ya leo tarehe 5 Shahrivar nchini Iran ni siku ya kumkumbuka Muhammad bin Zakaria Razi, msomi mtajika wa Kiislamu.

Muhammad bin Zakaria Razi alizaliwa mwaka 251 hijria katika mji wa Rei nchini Iran na alianza kujifunza kemia na fizikia akiwa bado kijana. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia.

Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi. Muhammad bin Zakaria Razi ameandika vitabu 56 vya tiba, 33 vya sayansi ya asili, 17 vya falsafa, 14 vya teolojia, 22 vya kemia na makumi ya vita katika nyanja mbalimbali.

Msomi huyo wa Kiislamu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 na alizikwa katika mji wa Rei ambao hii leo uko kusini mwa Tehran. 

Siku kama ya leo miaka 390 iliyopita, alifariki dunia Lope de Vega, mwandishi mkubwa wa Uhispania.

Vega alizaliwa mwaka 1562 Miladia na akiwa kijana mdogo alionekana kuwa mwenye harakati nyingi na mwenye kipawa kikubwa cha akili huku akianza pia kusoma mashairi.

Akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na shule ya msingi na sekondari ya kidini ambapo baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikuu, alijiunga na jeshi la kujitolea. Taratibu akaanza kuonyesha kipawa chake katika michezo ya kuigiza na masuala mengine na hivyo kuwavutia watu wengi. 

Lope de Vega anajulikana kuwa mwanzilishi wa michezo ya kuigiza kitaifa nchini Uhispania.   

Lope de Vega

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita, alizaliwa Georg Wilhelm Friedrich Hegel mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani.

Licha ya msomi huyo kufundisha katika vyuo mbalimbali na kuandika vitabu tofauti, lakini bado alikuwa masikini. Kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon dhidi ya Ujerumani mwaka 1806, Hegel alivutiwa na shakhsia ya kamanda huyo Kifaransa. Alibainisha hatua za historia na kuamiani kuwa, muelekeo wa harakati ya kihistoria huainishwa na Mwenyezi Mungu na kwamba hata malengo ya historia ni hivyo.

Katika kubainisha itikadi yake, Georg Wilhelm Friedrich Hegel  aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Hegel alifariki dunia mwaka 1831.

Georg Wilhelm Friedrich Hegel

 

Tarehe 27 Agosti mwaka 1896, kulitokea vita vya muda mfupi zaidi duniani visiwani Zanzibar.

Jengo la Kihistoria mjini Unguja linalojulikana kwa jina la Beit al-Ajaib lililojengwa na Sultan Barghash bin Said huko Forodhani kisiwani Unguja, lilishambuliwa kwa mizinga ya manowari za Uingereza. Hatua hiyo ilikuja kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wana wawili wa Sultani wa Zanzibar.

Watoto hao walijulikana kwa majina ya Said Barghash Khalid na Said Hamud bin Muhammed na ugomvi wao ulihusiana na utawala na nani anapaswa kurithi kiti cha ufalme. Vita hivyo vilidumu kwa dakika 45 tu na kuwa vita vifupi zaidi duniani.   ***

Tarehe tano Shahrivar miaka 47 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, mwanzo wa kalenda ya Iran ulirejeshwa tena katika mwaka wa Hijria Shamsia kutoka mwanzo wa tarehe wa Kifalme.

Katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu utawala wa kidikteta wa Pahlavi ambao ulitambua mafundisho ya Uislamu kuwa ni kinyume na maslahi yake, ulikuwa ukifanya njama za kukabiliana na Uislamu kwa kutumia utajiri na turathi ya kihistoria ya Iran.

Katika mkondo huo bunge la kimaonyesho la utawala wa Kipahlavi lilipasisha sheria iliyobadilisha mwanzo wa kalenda ya Iran kutoka mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) na kuifanya kuwa tarehe ya kuvikwa taji la Mfalme Kurosh wa silsila ya Khahamaneshi. Hatua hiyo ilikabiliwa na hasira na malalamiko makubwa ya Imam Ruhullah Khomeini na wananchi Waislamu wa Iran.

Kubadilishwa huko kwa mwaka wa Hijria na kufuata mwaka wa Kifalme nchini hakukudumu kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili na nusu na utawala wa Shah uliokuwa ukikabiliwa na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ulilazimika kutambua tena mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka kwenda Madina kuwa ndiyo mwanzo wa kalenda nchini Iran. 

Miaka 35 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Ali Akbar Kaveh, mwalimu mkubwa wa sanaa ya kaligrafia ya hati za Kifarsi.

Mtaalamu huyu alizaliwa mwaka 1271 Hijria mjini Shiraz, moja ya miji ya kusini mwa Iran na kuanza kujihusisha na masuala ya karigrafia. Baada ya hapo Ali Akbar Kaveh alipata kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo kama vile Mirza Twahir Katib, Homayun Hamedani na Imad Al Katib Seifi Qazwini na hatimaye akawa hodari mkubwa katika sanaa ya kaligrafia.   

Ali Akbar Kaveh

Na katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, yaani tarehe 27 Agosti mwaka 1991, nchi ya Moldova iliyoko mashariki mwa Ulaya ilipata uhuru.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia nchi hiyo ilikaliwa kwa mabavu na tawala, kaumu na nchi mbalimbali zikiwemo, Ukraine, Russia, Romania na utawala wa Othmania. Baada ya mapinduzi ya kikomunisti nchini Russia, Moldova iliungana na Romania.

Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moldova ilikaliwa kwa mabavu na Urusi. Hata hivyo baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo ikajikomboa na kupata uhuru.