Alkhamis, Agosti 18, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na 18 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, iliyopita, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama la kuchomwa moto Jumba la Sinema la Rex, watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti shirika hatari la ujasusi la Savak na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita kulifanyika mapinduzi ya Kimarekani dhidi ya serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq nchini Iran na baadaye kidogo Shah Reza Pahlavi akatwaa tena madaraka ya nchi. Mapinduzi hayo ambayo yalipangwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA kwa ushirikiano wa Uingereza, yaliiondoa madarakani serikali ya Musaddiq kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya wanaharakati wa kisiasa na wananchi na kueneza anga ya ghasia na machafuko nchini. Vilevile yalimrejesha Iran Shah Pahlavi ambaye siku tatu kabla alikuwa amekimbilia nchini Italia. Kabla ya tukio hilo la kusikitisha, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kukata mkono wa Uingereza hapa nchini na kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na wakoloni hao.
Siku kama ya leo miaka 937 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fakhir, msomi na mtaalamu mkubwa wa lugha wa Kiislamu mjini Baghdad. Akiwa kijana Ibn Fakhir alifanya safari mjini Makkah na Yemen na kukutana na maulama wakubwa wa zama hizo ambapo alitokea kuwa alimu mkubwa wa lugha na hadithi. Msomi huyo alitumia njia ya kufikisha ujumbe kupitia mashairi yaliyokuwa na ufasaha wa hali ya juu. Miongoni mwa athari za Ibn Fakhir ni pamoja na kitabu kinachoitwa ‘Jawaabul-Masaail.’
Na siku kama ya leo miaka 1363 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.