Jumatano, Agosti 31, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 28 Dhulqaada Mfunguo Pili 1437 Hijria sawa na 31 Agosti 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita karibu Waislamu 1,000 wa Iraq waliokuwa katika shughuli ya maombolezo kwenye mji mtakatifu wa Kadhimain, waliuawa. Siku hiyo karibu Waislamu milioni moja wa madhehebu ya Shia walikuwa katika maombolezo ya kukumbuka siku ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Mussa al-Kadhim (as). Milipuko kadhaa ya mabomu iliyotokea katika eneo la maombolezo hayo iliwatia hofu waombolezaji hao ambao walianza kukimbia huko na kule na baadhi yao kuanguka chini na kukanyagwa hadi kufa. Baadhi ya wahanga wa tukio hilo pia walianguka kutoka kwenye daraja maarufu la Aimma lililoko katika mji huo wa Kadhimain.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kufahamu hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda.
Na siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ya Malaysia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Wananchi wa Malaysia walianza kuingia taratibu katika dini ya Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa nchi za Ulaya ulianza kuenea nchini humo mwanzoni mwa karne ya 16 sambamba na kuwasili nchini humo baharia wa Kireno, Albuquerque. Uholanzi iliidhibiti nchi hiyo katika karne ya 17 na kuanza kuikoloni. Mwaka 1824 nchi za Uholanzi na Uingereza zilifikia makubaliano ambapo Waingereza waliichukua Malaysia na Waholanzi wakachukua Indonesia. Waingereza waliendelea kuikolonia Malaysia hadi nchi hiyo ilipopata uhuru katika siku kama ya leo.