Aug 31, 2016 23:06 UTC
  • Alkhamisi, Septemba 1, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na tarehe Mosi Septemba 2016.

Siku kama ya leo miaka 842 iliyopita, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu yake. Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda kwa karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umefanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali.

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita yaani tarehe Mosi Septemba mwaka 1939, Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi kuanzisha mashambulizo dhidi ya Poland. Adolf Hitler alianza kuliandaa jeshi lenye nguvu wakati akiwa madarakani huko Ujerumani kwa kutumia vibaya hadhi yake na hisia za ubaguzi na utaifa wa wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wamefedheheka sana kufuatia kushidnwa vibaya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi kifupi, Hitler alifanikiwa kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika.

Siku kama leo miaka 55 iliyopita, yaani sawa na tarehe Mosi Septemba  mwaka 1961, ulifanyika mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Isiyofungamana na Upande Wowote NAM huko Belgrade mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 duniani. Jumuiya ya NAM iliasisiwa lengo kuu likiwa ni kuziunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu mkabala na kambi za Mashariki na Magharibi. Masharti makuu ya kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa mwanachama rasmi katika muungano unaofungamana na madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo Kanali Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya, alichukua madaraka ya nchini hiyo kupitia mapinduzi ya kijeshi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa chini ya mfumo wa Kisultani huku mfalme Idriss wa Kwanza akiongoza nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Na tarehe 19 Shahivar miaka 55 iliyopita mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 7.3 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika eneo la Buin Zahra huko kaskazini magharibi mwa Iran. Mtetemeko huo mkubwa uliua zaidi ya watu elfu 20 na kujeruhi maelfu ya wengine. Mtetemeko huo wa ardhi ulitokea nyakati za usiku na hivyo haukuwapa watu fursa ua kuokoa maisha yao.

Mtetemeko huo wa Buin Zahra uliharibu kabisa vijiji 120 na kusababisha hasara kubwa katika mamia ya nyumba za eneo hilo. Baada tu ya mtetemeko huo wananchi wa Iran waliharakia kuwapelekea misaada wenzao wa Buin Zahra.