Sep 02, 2016 23:11 UTC
  • Jumamosi tarehe 3 Septemba, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhul-Hijja mwaka 1437 Hijria mwafaka na tarehe 3 Septemba mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatima binti ya Mtume SAW alianza maisha mapya baada ya kufunga ndoa na Imam Ali bin Abi Talib AS. Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema, mtukufu na kigezo bora cha wanawake na Waislamu kwa ujumla. Masahaba mashuhuri walijitokeza kumposa binti huyo wa Mtume. Hata hivyo, Mtume alikuwa akimjibu kila aliyekwenda kumposa binti yake huyo kwamba, suala la ndoa yake liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao walianza maisha yao ya kawaida kabisa yaliyojaa huruma, upendo na masuala ya kiroho na kimaanawi. Familia hiyo imeitunuku dunia shakhsia adhimu na wa kupigiwa mfano kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as). ***

Katika siku kama ya leo miaka 852 iliyopita yaani tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhul-Hijja mwaka 586 Hijria alizaliwa Ibn Abi al-Hadid mwanazuoni na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Alikuwa mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Muutazila, fakihi, mshairi, mwandishi na mwanateolojia. Kitabu chake cha Sharh ya Nahaj al-Balagha ambacho kimempa umashuhuri maalumu kinaonyesha mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa Amir al-Muuminina na familia ya Bwana Mtume SAW. Kitabu cha Nahjul Balaghah kimekusanya, semi za hekima, barua na hotuba za Imam Ali bin Abi Twalib (AS). Katika kitabu hicho Ibn Abil Hadid amefanya jitihada kubwa kuonyesha adhama ya Nahjul Balagha kwa kuzingatia fasihi, historia na ufasaha wa lugha. ***

Miaka 358 iliyopita katika siku kama ya leo, Oliver Cromwell Rais wa kwanza na wa mwisho wa Uingereza aliaga dunia. Alianza harakati za kisiasa na kijamii katika rika lake la ujana na mwaka 1640 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Bunge. Katika zama hizo Charles I ndiye aliyekuwa mfalme wa Uingereza.***

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hat hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake Damascus ilidhibitiwa na Ufaransa. ***

Miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza viliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hiterl pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poand bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo. ***

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita. ***

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, maandamano ya kwanza ya mamilioni ya wananchi wa Waislamu dhidi ya utawala wa Shah yalifanyika. Maandamano hayo yalifanyika kwa mnasaba wa Sikukuu ya Eid al-Fitr. Maandamano hayo yalianza baada ya Swala ya Idi katika nukta nne za mji wa Tehran na hatua kwa hatua watu wakawa wanajiunga na maandamano hayo. Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba picha za Imam Khomeini MA walikuwa wakitoa nara za kutaka uhuru, kujitawala na kuweko mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Maandamano hayo kwa hakika yaliandaa mazingira ya maandamano ya kihistoria yaliyofanyika mwaka huo huo. ***