Jumatano, Septemba 7, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 5 Mfunguo Tatu Dhilhija 1437 Hijria sawa na Septemba 07, 2016.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu bila ya kuzingatia hali hiyo, wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.
Tarehe 5 Dhulhija miaka 76 iliyopita, alifariki dunia huko Najaf, Iraq Allamah Muhammad Hussein Kampani, mwanafalsafa, faqihi na arifu mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1296 Hijria mjini Kadhimain nchini Iraq. Msomi huyo mkubwa pia alitabahari katika elimu za falsafa, tiba, irfan, historia, jografia, mashairi na fasihi. Mbali na hayo Allamah Kampani alikuwa na fikra pevu na uwezo mkubwa wa kubainisha mambo. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa katika nyanja mbalimbali ikiwemo diwani ya mashairi akisifu viongozi wa Uislamu.
Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru wake toka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo nchini humo.
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita kulitokea Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Hata hivyo Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo.