Sep 09, 2016 03:43 UTC
  • Ijumaa, Septemba 9, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 07 Dhilhija mwaka 1437 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Septemba 2016.

Tarehe 7 Dhulhija miaka 1323 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir" yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).

Siku kama hii ya leo miaka 187 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Miaka 40 iliyopia katika siku kama ya leo, aliaga dunia Mao Tse Tung kiongozi wa Uchina. Tse Tung alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza juu ya kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita Ahmad Shah Masoud mmoja wa makamanda wakubwa wa Mujahidina wa Afghanistan ambaye pia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya mpito ya Rais Burhanuddin Rabani wa Afghanistan, aliuawa. Ahmad Shah Masoud alizaliwa mwaka 1952 na alianza kupigana vita na nchi za kigeni katika milima ya kaskazini mwa Afghanistan sambamba na kuingia madarakani wakomunisti huko Afghanistan na mara baada ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na jeshi la Urusi ya zamani mwaka 1979.