Jumamosi Septemba 10 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1437 Hijria mwafaka na tarehe 10 Septemba mwaka 2016 Miladia.
Leo tarehe 8 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja ni siku ya tarwiya. Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikani katika jangwa na Arafa na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafa kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa.
Katika siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume SAW aliondoka Makka na kuelekea katika mji wa Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka katika pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazid za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka mjini Kufa.
Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya ziwa la Mazury. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi waitifaki. Katika vita hivyo vya Mazury, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walipata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika VitaVikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi liliharibu kabisa mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 na watu 10,000 wakapoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo pia ulitoa pigo kubwa kwa miundombinu ya uchumi wa nchi hiyo.
Na katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Samuel Kanyon Doe Rais wa wakati huo wa Liberia aliuawa na vikosi vya waasi. Aliingia madarakani mwaka 1980 kwa mapinduzi ya umwagaji damu akitumia malalamiko ya umasikini na kutoridhishwa wananchi wa nchi hiyo na bei ya juu ya bidhaa. Utawala wa Samuel Doe sio tu kwamba, haukuweza kupunguza masaibu ya umasikini ya wananchi wa Liberia, bali ulizusha hitilafu za kikabila na kuiongezea nchi hyo matatizo ya kiuchumi na kijamii. Aidha hatua yake ya kupanua ushirikiano na Marekani na utawala haramu wa Israel uliifanya nchi hiyo iwe tegemezi na kuandaa mazingira ya kuporwa madini ya almasi.