Sep 11, 2016 01:28 UTC
  • Jumapili, Septemba 11, 2016

Leo ni Jumapili tarehe tisa Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah mwaka 1437 Hijiria mwafaka na Septemba 11, 2016 Miladia.

Leo ni tarehe tisa Dhul-Hijjah ambayo ni siku ya Arafah, moja ya siku tukufu kwa Waislamu inayotambulika pia kuwa ni Iddi. Katika siku kama hii Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaalika waja wake kwa ajili ya ibada na twaa yake huku naye akiwaandalia kheri na baraka. Aidha katika siku hii ya leo shetani hudhalilika na kupata hasira kali. Tangu adhuhuri ya tarehe tisa Dhul-Hijjah mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu husimama katika jangwa la Arafah ambapo hupata fadhila nyingi kwa kisimamo hicho. Arafah ni jina la jangwa pana lenye bonde na mlima unaoitwa 'Jabalur-Rahmah' yaani mlima wa rehema, huko kusini mashariki mwa mji wa Makkah. Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa  kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili ya amali nyingine za Hija.

 

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea mjini al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba walikuwa tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake.

Siku kama ya leo miaka 789 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 mfasiri wa Qur'an Tukufu

 

Abu Ali Fadhl Bin Hassan Twabarsi alizaliwa mwaka 468 Hijiria. Baada ya kusoma masomo ya msingi huko mjini Mash'had, alianza kujifunza lugha ya Kiarabu, kisomo cha Qur'an, tafsiri, hadithi, hisabati, fiqhi, usulu fiqhi na theolojia ya dini ya Kiislamu. Kwa miaka karibu 54 msomi huyo aliishi mjini Mash'had na baadaye akaelekea mjini Sabzawar na kujishughulisha na ufundishaji. Wasomi wakubwa wa Kiislamu kama vile, Qutubuddin Rawandi, Ibn Shar Ashub, Dhiya'uddin Rawandi na wengineo, ni miongoni mwa wanafunzi wa Allamah Twabarsi. Aidha vitabu kama vile 'Asraarul-Imamah' 'Taajul-Mawaaliid' 'Kunuzun-Najaah' na 'Tafsir Maj'maul-Bayaan' ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo.

 

Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa nchi ya Pakistan

 

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, alifariki dunia, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India.

Mashambulizi ya Septemba 11 Marekani

 

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita yaani tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege nyingine ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuanguka. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.