Sep 11, 2016 22:07 UTC
  • Jumatatu 12 Septemba 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Dhilhija 1437 Hijria sawa na 12 Septemba 2016 ambayo ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu.

Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka, huchinja mnyama kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola wao na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Mtukufu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu aliijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mwanawe kipenzi Ismail (as). Licha ya mashaka ya utekelezwaji wa amri hiyo, Nabii Ibrahimu (as) aliandaa mazingira ya kutekeleza amri hiyo na kumlaza chini mwanaye na kuanza kuikata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja. Hapo ndipo alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amefaulu mtihani huo na akamtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawapa wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita yaani 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baba na mama yake walikuwa wasomi mahiri katika fizikia. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mionzi ya nururishi au radioactive.

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Sellasie. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na kisha baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia ili ayafanye yawe chini ya utawala wake. Haile Selassie aliwaahjiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya mabadiliko ya kiofisi hatua kwa hatua. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1953 yalisitisha mpango wake huo.

Na tarehe 10 Dhilhija mwaka mmoja uliopita katika sikukuu ya Idul Haji maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu walipoteza maisha katika eneo la Mina wakitekeleza ibada ya Hija. Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea asububuhi saa tatu wakati maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu walipokuwa wakielekea kwenye ibada ya kumpiga mawe Shetani. Wakati huo askari wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia walifunga baadhi ya barabara zinazoelekea kwenye eneo la ibada hiyo, suala ambalo lilisababisha msongamano mkubwa na hatimaye mahujaji zaidi ya elfu saba wakapoteza maisha katika hali ya kusikitisha. Mahujaji zaidi ya 464 wa Iran pia walipoteza maisha yao katika tukio hilo lililodhihirisha uzembe na kushindwa kwa serikali ya Saudia kusimamia ipasavyo ibada ya Hija. Tukio hilo ni miongoni mwa matukio machungu zaidi katika historia ya ibada ya Hija.