Sep 14, 2016 23:54 UTC
  • Zilzala ya Tabas
    Zilzala ya Tabas

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Dhulhija 1437 Hijria inayosadifiana na 15 Septemba 2016.

Tarehe 25 Shahrivar yaani siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha Rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando ya mji huo. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita alifariki dunia Sheikh Agha Bozorg Tehrani, fakihi na mtambuzi mkubwa wa vitabu wa Kiislamu. Sheikh Muhammad Hassan Razi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Agha Bozorg Tehrani alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye akaelekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika mji huo mtakatifu alihudhuria masomo na darsa za maulama mahiri wa zama hizo kama Akhund Khorasani na Mirza Hussein Nouri na akafanikiwa kupata daraja ya Ijtihad. Miongoni mwa huduma kubwa zilizotolewa na mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni kitabu chake cha "al Dhari'a fii Tasanifi Shia". Mwanazuoni huyo amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.

Siku kama hii ya leo miaka 100 iliyopita, alizaliwa mwandishi na mtafiti wa Kiromania, Constantin Virgil Gheorghiu. Virgil alianza kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali ikiwemo dini ya Kiislamu baada ya kuhitimu masomo. Kitabu chake alichokipa jina la "Mtume Muhammad" ni moja kati ya kazi zake mashuhuri za uandishi zilizopongezwa na kusifiwa katika ulimwengu wa Kiislamu hususan nchini Iran. Constantin Virgil alifariki dunia mjini Paris, Ufaransa mwaka 1992.

Na miaka 195 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi kadhaa za America ya Latini zilijiondoa katika ukoloni wa Uhispania. Nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilikuwa chini ya utawala wa Uhispania tangu mwanzoni mwa karne ya 16. Wimbi la kupigania uhuru katika eneo hilo lilianza mwanzoni mwa karne ya 19 na kuanza kuelekea kwenye uhuru baada ya kudhoofika serikali kuu ya Uhispania. Uasi wa wananchi wa maeneo hayo ulizaa matunda na hatimaye tarehe 15 Septemba mwaka 1821 ulitangazwa uhuru wa nchi hizo. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati.