Sep 17, 2016 23:13 UTC
  • Msikiti wa Cordoba
    Msikiti wa Cordoba

Leo ni Jumapili tarehe 16 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah mwaka 1437 Hijiria, mwafaka na Septemba 18, 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 966 iliyopita, alifariki dunia Abu Abdillah Muhammad Jiyani, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu huko Andalusia, Uhispania. Ibn Jiyani alizaliwa mwaka 379 Hijiria mjini Córdoba, moja ya miji ya zamani ya Uhispania ambapo alipata kusoma elimu ya msingi mjini hapo. Hatimaye alielekea mjini Cairo, Misri na kuishi kipindi cha miaka minne. Ibn Jiyani alikuwa mtaalamu mkubwa katika fani ya nujumu na hisabati. Ameacha athari kadhaa katika uwanja huo.

Katika siku kama ya leo miaka 307 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa michezo ya kuigiza, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, Johnson alijiunga na Chuo Kikuu cha Oxford, hata hivyo kutokana na hali ngumu ya kimaisha aliyokuwa nayo alikatisha masomo. Akiwa na umri wa miaka 28 alielekea mjini London, Uingereza na kuanza kuandaa makala za kisiasa na katika uga wa fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, alifariki dunia Leonhard Euler, mwanahisabati mkubwa wa nchini Uswisi. Euler alizaliwa tarehe 15 April mwaka 1707 mjini Ball na akiwa mdogo alipendelea sana fani ya hisabati ambapo alijiunga na Chuo kikuu cha Ball nchini humo. Umashuhuri wa Leonhard Euler ulianza akiwa na umri wa miaka 19 ambapo kipindi hicho chuo cha akademia cha Paris kiliandaa shindano huku makala ya Euler yakishika nafasi ya pili. Miaka kadhaa baadaye alifanya safari nchini Russia na Ujerumani na kujiendeleza kielimu zaidi. Aidha anafahamika kama mchapakazi na aliyekuwa na athari kubwa katika zama zake. Ameacha athari nyingi katika uwanja wa hisabati ambazo baadhi zinapatikana katika maktaba kubwa.

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, nchi ya Chile ilijipatia uhuru wake. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa kwake, Chile ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru. Mwaka 1788 na katika kuandaa makoloni yake Charles III, mfalme wa Uhispania aliamua kuitenga kwa kiasi kidogo Chile kutoka Peru. Ni baada ya hapo ndipo mwamko wa kupigania uhuru wa raia wa Chile ulipoanza mwaka 1814 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa. Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka. Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani.