Jumatano, Septemba 21, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 19 Dhulhija 1437 Hijria sawa na 21 Septemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah, mwanasiasa na mwasisi wa uhuru wa Ghana. Nkurumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya Ghana kupatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.
Na siku kama ya leo miaka 22 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.
siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na ardhini dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.