Sep 21, 2016 07:22 UTC
  • Familia Salama (9)

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia kuhusu vitabu na usomaji vitabu katika familia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Vitabu na usomaji vitabu kwa jamaa katika familia ni jambo ambalo daima limekuwa na umuhimu mkubwa. Kwa kawaida watoto huanza kusoma wakifika umri wa miaka sita na juu. Pamoja na hayo pia kuna uwezekano wa watoto kupenda kusoma vitabu wakiwa na umri wa miaka ya chini na hili huwezekana hasa iwapo wazazi wenyewe ni wenye kupenda kusoma vitabu mara kwa mara.
Katika kundi la watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, watoto huhitajia vishawishi vya kusoma kupitia vitabu vyenye rangi rangi ili waweze kuwajua watu, mimea, wanyama n.k. Katika umri huu watoto huhitajia vitabu vyenye kurasa ngumu zisizopasuka kirahisi na zenye picha za kuvutia.
Kwa watoto walio na umri wa miaka 6 hadi 9, huhitaji vitabu vyenye hadihiti fupi fupi na zenye kuvutia. Wazazi wanaweza kuwauliza watoto mtazamo wao kuhusu wanayoona au kusoma katika kitabu ili kwa njia hiyo waboreshe uwezo wa watoto kutafakari na kuchambua mambo. Hali kadhalika watoto wanaweza kufafanua kuhusu hadithi zilizo katika vitabu kwa maneno yao wenywe.
Kwa kutumia mbinu hii wazazi wanaweza kutathmini namna watoto wao wanavyostawi kwa mtazamo wa mantiki, kuhifadhi na pia umahiri wao katika kufahamu au kudiriki mambo. Taswira au picha katika vitabu huwasaidia watoto kuweza kudiriki hadithi na kuzikumbuka.

 

Watoto walio na umri wa miaka 10 na mabarobaro, huanza kutafuta maudhui ngumu zaidi ambazo zinaenda sambamba na umri wao na hufurahi na kuburudika na yale wanayojifunza.
Hupenda shakhsia au mhusika wa hadithi mwenye kujibu matakwa yao. Wakiwa katika umri huo hupata taswira za kimaadili na kimaannawi na mtazamo wao kuhusu dunia huanza kuibuka.
Kadiri watoto wanavyokuwa wakubwa, huanza kuwa na mtazamo huru kuhusu vitabu wanavochagua kuvisoma. Kwa msingi huo wazazi wanapaswa kuchukua tahadhari na kuzingatia vitabu ambavyo watoto wao wanasoma. Iwapo mzazi atampata barobaro anasoma kitabu kishochofaa hapaswi kuchukua hatua ya hamaki ya kumkataza mara moja bali anapaswa kufanya mazungumzo naye. Hii ni kwa sababu kumkataza barobaro kusoma kitabu bila kuwepo mazungumzo ya kumkinaisha yamkini kusiwe na faida.
Wazazi wanaweza kuwaarifishia watoto wao vitabu vizuri vya kusoma visiivyo vya hadithi kama vile vya jiografia, historia ya kisasa, sayansi za kuvutia, maajabu ya dunia n.k ili watoto wazoee kusoma vitabu vyenye kuwafaidi sambamba na kutambua na kuifahamu dunia inayowazunguka.
Njia mojawapo ya kupata vitabu vizuri vya kusoma ni kupitia maduka ya vitabu au kushauriana na wachapishaji ambao hufika katika maonyesho ya vitabu ambayo hufanyika katika miji mbali mbali duniani. Hali kadhalika wazazi wanaweza kuwasaidia watoto kupata vitabu kupitia utafutaji katika intaneti ambapo pia kuna maduka ya kiintaneti ya kuuza anuai ya vitabu.
Mbali na kuwasaidia watoto kuchagua vitabu vinavyofaa vya kusoma, wazazi wanapaswa pia kuwaonyesha watoto mbinu za usomaji sahihi ili waweze kufurahia na kuvutiwa na wanayoyasoma ili kwa njia hiyo waweze kujifunza mengi wakati wa kusoma vitabu hasa vitabu vya masomo ya shuleni.
Moja ya mbinu muafaka za kuimarisha kiwango cha kujifunza wakati wa kusoma kitabu au mutalaa ni kuandika nukta muhimu katika daftari.
Kuandika nukta za kuvutia na muhimu katika kitabu hupelekea mwenye kusoma kujifunza na wakati wa kusoma mara ya pili maudhui hiyo anaweza kurejea katika nukta alizoziandika na hivyo kupunguza wakati ambao angetumia kusoma kitabu chote upya.
Mbinu nyingine ya mutalaa wa vitabu ni kuandika pembeni mwa kitabu unachokisoma, aghalabu kwa kutumia penseli ili uweze kufuta baadaye. Mbinu hii humuwezesha msomaji kufanya mutalaa mara ya pili kwa njia rahisi kwa kuangazia nukta muhimu.
Mbinu nyingine inayofaa katika mutalaa ni kubaini maneno muhimu ya maudhui husika. Aina hii ya mutalaa huwa yenye kutegemea msingi wa ufahamu wa maudhui kwa ujumla na si kuhifadhi tu bila kudiriki maana.
Wataalamu wa elimu wanasema mbinu hii ya kuchagua neno muhimu katika maudhui husaidia kudiriki na kufahamu na ni mbinu bora zaidi na kamilifu kuliko mbinu zinginezo.
Mutalaa kwa kutumia mbinu sahihi humsaidia msomaji kufahamu na kuhifadhi mambo kwa muda mrefu. Iwapo mwenye kusoma ataweza kuhifadhi anayoyasoma basi jambo hili huimarisha utamu wa mutalaa na kumuwezesha mwanafunzi kujifunza mengi na hivyo kumfanya awe na hamu ya kusoma vitabu zaidi.
Kwa ujumla ni kuwa mbali na kusoma vitabu kwa ajili ya masomo ya shule, madrassah au chuo kikuu, yaani kusoma kwa ajili ya mitihani, kuna haja ya kuwa na mazoea ya kusoma vitabu kwa ajili ya kujiburudisha au kuzidisha maarifa.
Kuna haja kwa walezi na wazazi kuwanunulia vitabu watoto wao ili kuwajengea utamaduni wa kupenda kujisomea vitabu vya ziada na kiada ili kukuza uelewa wao.
Katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Afrika Mashariki kumeshuhudiwa ongezeko la tamasha za kuwahamasisha watoto umuhimu wa kusoma vitabu sambamba na kupanuliwa wigo wa upatikanaji wa vitabu vya watoto. Nukta hii ni chanya na inaonyesha kuna hatua zinazochukuliwa kuimarisha na kustawisha utamaduni wa kusoma. Tarehe 28 Aprili imetangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa siku ya Kimataifa ya vitabu na hati miliki.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO limekuwa likiadhimisha siku hii kila tarehe 23 April kwa miaka takribani 20. Nchi wanachama wa UNESCO huadhimisha siku hii kwa kutambua umuhimu na uwezo wa vitabu katika kuwaleta watu pamoja na kuelimisha kuhusu utamaduni wa watu na ndoto zao za mustakbali bora hapo baadaye. Siku hii ni mahsusi kwa ajili ya kuchangia elimu na usomaji , lakini pia kulinda hati miliki ya upatikanaji na utajiri wa vitabu duniani.
Wapenzi wasikilizaji tunafikia tamati ya makala yetu ya leo kwa kumnukulu Kiongozi wa Waumini, Imam Ali AS aliposema:
Yule ambaye anapata utulivu katika vitabu, basi hawezi kupokonywa utulivu na starehe hiyo.