Alkhamisi 22 Septemba 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Dhulhija 1437 Hijria sawa na 22 Septemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizaliwa katika eneo la Khomeini. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.
Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita yaani tarehe 22 Septemba mwaka 1828, Shaka Zulu kiongozi na mwasisi wa utawala wa Kifalme wa Zulu nchini Afrika Kusini aliuawa na ndugu zake wawili wa kambo. Shaka aliliongoza kabila kubwa la Zulu tangu mwaka 1815 na katika kipindi kifupi aliweza kuyaweka chini ya uongozi wake maeneo mengi ya Afrika Kusini. Baada ya kuuawa Shaka, kaka yake mmoja alichukua hatamu za uongozi na kuanzia mwaka 1830 hadi 1839 akapigana na wahamiaji wa Kiholanzi waliojulikana kama Boers. Hatimaye serikali ya Shaka ilipata pigo kutoka kwa Uingereza mwaka 1880 na kugawanyika katika serikali kadhaa ambazo hazikuwa na mamlaka kamili.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.