Sep 23, 2016 02:52 UTC
  • Ijumaa 23 Septemba, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Dhulhija 1437 Hijria sawa na Septemba 23, 2016.

Miaka 37 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath wa Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Nchi hiyo ina miji mitakatifu ya Makka na Madina na Mtume wa Uislamu Muhammad SAW alizaliwa katika mji wa Makka. Tangu mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria, Saudi Arabia iliondoka chini ya himaya ya utawala wa Bani Abbas na hali ya mambo ya nchi hiyo haikuwa shwari kwa karne kadhaa. Serikali ya Othmania iliivamia Saudi katika karne ya 16 Miladia na kuanzia katikati mwa karne ya 17 ukoo wa Aal Saud ulianza kufanya juhudi za kuiongoza nchi hiyo na jitihada hizo ziliendelea hadi mwanzoni mwa karne ya 20.

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria. Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

Na miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 21 Dhulhija mwaka 1329 Hijiria, alifariki dunia Ayatullah Aakhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani, mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu wa Iran. Baada ya kuhitimu elimu yake ya mwanzo, msomi huyo alisoma katika vyuo vya kidini mashuhuri vya zama zake na kufuzu vyema. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na miongoni mwao ni kitabu muhimu cha 'Kifayatul Usul' ambacho hadi sasa ni kati a vitabu vyenye hadhi kubwa katika somo la usuulul fik'hi kwenye vyuo mbalimbali vya kidini.