Jumamosi, Septemba 24, 2016
-
Sehemu alipozikwa Sahaba wa Mtume Muhammad SAWA, Maytham al-Tammar
Leo ni Jumamosi tarehe 22 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1437 Hijria mwafaka na tarehe 24 Septemba mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib AS aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa na Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na Ubaidullah ibn Ziyad kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). ***
Miaka 196 iliyopita katika siku kama ya leo, duru ya pili ya vita kati ya Iran na Russia ilianza. Chanzo cha vita hivyo ilikuwa ni hatua ya vikosi vya Russia ya kuvamia kijeshi maeneo ya mpakani ya Iran. Licha ya wanajeshi wa Iran kujitolea mno katika vita hivyo, lakini kutokana na udhaifu wa serikali kuu na kutopatiwa msaada kwa wakati walishndwa katika vita hivyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita alizaliwa Konstantin Chernenko kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti kabla ya Mikhail Gorbachev. Akiwa na umri wa miaka 18 alikuwa kiongozi katika Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Kikomonisti. Baada ya Konstantin Chernenko kufariki dunia, Mikhail Gorbachev alimrithi kiti cha uongozi wa Umoja wa Kisovieti. ***
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, ndege za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio ya mabomu katika mji mkuu wa Poland Warsaw. Mashambulio hayo ya mabomu yalidumu kwa muda wa siku tatu wakati wa kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Duni. Adolph Hitler, Kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi alikuwa ametoa amri ya kudhibitiwa mji huo kwa gharama yoyote ile. ***
Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry na mrithi wa kiti cha Ufalme wa Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18.