Sep 27, 2016 02:27 UTC
  • Jumanne, Septemba 27, 2016

Leo ni Juumanne tarehe 25 Dhulhaji 1437 Hijria sawa na tarehe 27 Septemba 2016.

Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as). Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo.

Leo tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Utalii Duniani. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki kwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Siku kama leo miaka 20 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi.