Jumatano, Septemba 28, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 26 Dhulhija 1437 Hijria sawa na Septemba 28, 2016.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sanjari na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia Misri. Hatua ya viongozi wa Misri ya kujibu hujuma hiyo, iliongeza umaarufu wa Abdel Nasser nchini Misri na ulimwenguni kwa ujumla.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin. Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege. Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Azimio hilo lililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo.
Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa na utawala huo ghasibu, ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa Israel na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel.
Siku kama ya leo miaka 878 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq Abul-Fadhail Amedi, fakihi na mwanafasihi wa Kiislamu. Baada ya kusoma elimu za fiqhi, usul fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo. Abul Fadhail Amedi alikuwa na mashairi yenye kubeba maana kubwa. Amedi aliaga dunia mwaka 608 Hijria akiwa katika eneo alilozaliwa akiwa na umri wa miaka 49.