Oct 03, 2016 08:20 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 13, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 3, 2016.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu.    

Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka kwenda Madina

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita yaani tarehe Mosi Muharram mwaka wa 7 tangu Mtume (saw) abaathiwe na kupewa utume kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu, Makuraishi walifunga mkataba wa kuweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake. Viongozi wa makafiri wa Makka ambao walikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kasi ya kustawi Uislamu na vilevile kutokana na kufeli njama zao za kuzuia kuenea dini hiyo, waliamua kuweka mzingiro wa kiuchumi ili kufanikisha malengo yao. Kwa msingi huo waliamua kuweka mkataba dhidi ya Waislamu. Mkataba huo uliwakataza watu wote kufanya muamala wa aina yoyote na wafuasi wa dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake walizingirwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika bonde lililojulikana kwa jina la Shiibi Abi Twalib wakisumbuliwa na matatizo mengi na mashinikizo ya kiuchumi na katika kipindi hicho Mtume (saw) alipoteza wasaidizi wake wawili muhimu yaani ami yake, Abu Twalib na mkewe kipenzi, Bibi Khadija. Waislamu hao walisimama imara kulinda imani yao na hawakutetereka hata kidogo licha ya matatizo makubwa waliyokabiliana nayo. Mzingiro huo wa kiuchumi dhidi ya Waislamu ulikomeshwa mwezi Rajab mwaka wa kumi baada ya kubaathiwa Mtume.

Ramani ya sasa ya eneo la Shiibi Abi Twalib

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, baada ya Imam Khomeini MA kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq na kutokana na mashinikizo ya utawala wa zamani wa Baghdad mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alilazimika kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait. Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah. Kufuatia hatua hiyo, siku kadhaa baadaye Imam Khomeini MA alielekea uhamishoni nchini Ufaransa. Itakumbukwa kuwa, miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq, vilizusha hasira za wananchi wa Iran, ambao walikuwa katika siku muhimu za kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini.

Imam Khomeini akiondoika Iraq kwenda Paris

Tarehe Mosi Muharram miaka 38 iliyopita watu 300 waliokuwa na silaha walianzisha harakati kubwa ya silaha dhidi ya utawala wa kifalme wa Aal Saud huko Saudi Arabia kwa kuvamia na kuukalia Msikiti Mtukufu wa Makka. Harakati hiyo iliyonzishwa baada ya kumalizika ibada ya Hija, iliongozwa na raia wa Saudia aliyejulikana kwa jina la Juhayman al-Otaibi. Harakati hiyo iliendelea kwa kipindi cha wiki mbili na hatimaye askari wa Saudi Arabia wakisaidiwa na kikosi maalumu cha jeshi la Ufaransa, walishambulia Msikiti Mtukufu wa Makka na kukatokea mapigano makali yaliyopelekea kuuawa watu 244 kutoka pande zote mbili. Mwezi mmoja baada ya tukio hilo waasi wengine 36 walikatwa vichwa na utawala wa Aal Saud.

Juhayman al-Otaibi

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, umoja mpya wa Ujerumani ya Mashariki na Ujerumani ya Magharibi ulitangazwa rasmi na nchi mbili hizo kwa mara nyingine tena zikaunda Ujerumani moja baada ya miaka 45 ya kutengana. Baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa Ujerumani lilikaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani na lile la magharibi likadhibiwa na nchi za Magharibi. Nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na ya Mashariki zilitangazwa kuasisiwa mwaka 1949 kwa kuwa na mifumo miwili tafauti ya kisiasa na kiuchumi.

Bendera ya Ujerumani

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, wawakilishi wa Italia na utawala wa kifalme wa Austria walisaini mkataba wa Vienna katika mji unaojulikana kwa jina hilo. Kwa mujibu wa mkataba huo, Austria iliikabidhi Italia jimbo la Venice. Moja kati ya vipengee muhimu vya mkataba wa Vienna kilikuwa ni hiki kwamba, utawala wa kifalme wa Austria upigwe marufuku kuingilia masuala ya ndani ya Italia. Mkataba wa Vienna ulifungua njia ya kuungana Italia mwaka 1870.

Mkataba wa Vienna

Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia. Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ukachaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.

 

Bendera ya Iraq