Oct 04, 2016 01:03 UTC
  • Jumanne, Oktoba 4, 2016

Leo ni Jumanne tarehe Pili Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 4, 2016

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya.

Tarehe 4 Oktoba miaka 186 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.

Bendera ya Ubelgiji

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputnik 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.

Satalaiti ya kwanza kurushwa angani

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, ilivumbuliwa dawa ya penicillin na tabibu Alexander Fleming. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.

Alexander Fleming

Na tarehe 4 Oktoba mwaka 1963 yaani miaka 53 iliyopita kimbunga cheusi cha Caribbean kilianza na kuangamiza suhula zote za bandari na visiwa vya bahari ya Caribean. Kimbunga hicho angamizi kilikuwa na kasi ya kilomita 150 kwa saa na kwa ujumla kiliua karibu watu elfu sita wengi wao wakiwa raia wa Cuba na Haiti.